LIGI Kuu Bara inazidi kuwa ya moto kuelekea mwishoni mwa msimu kila timu ikibakiza
michezo tisa kumaliza kazi yake.
Wakati kila timu ikiwa imeshacheza michezo 21, zipo timu ambazo zinaonekana kufanya vizuri katika idara tofauti na nyingine hali inaonekana sio shwari licha ya kuwa katika nafasi tofauti.
Kuna timu zilizofunga mabao mengi kama Simba imefunga 51, Yanga 39 na Azam FC 36 lakini zipo timu zimefungwa mabao machache zikiongozwa na Yanga 10, Simba 12 na Singida Big Stars 15 na wengine waliobaki wamefungwa mabao kuanzia 21.
Zipo timu zimefungwa mabao mengi kuliko zingine kwenye Ligi Kuu na ukizitazama nafasi zilizopo bado pia hazina uhakika sana wa kubaki salama kutokana na utofauti wa pointi kutoka kwa mmoja kwenda kwa mwingine kuwa mkubwa.
MTIBWA SUGAR
Mtibwa Sugar inaonekana iko vizuri msimu huu kuliko mingine mitatu iliyopita baada ya kunusurika mara kadhaa kushuka daraja. Msimu huu wanaonekana kujitahidi ingawa bado kiwango chao sio cha kuridhisha sana kwa hivi karibuni.
Mtibwa ni miongoni mwa timu nne ambazo zinaongoza kwa kufungwa mabao mechi kuliko ya kufunga ikionesha dhahiri safu yao ya ulinzi sio bora sana. Katika michezo 21 iliyokwishacheza imeshinda sita, wamepata sare saba na kupoteza nane wakiwa kwenye nafasi ya nane kwa pointi 25.
Timu hiyo imefunga mabao 24 na imeruhusu kufungwa mabao 32 ikionesha kuna tatizo, licha ya kuwa katika nafasi nzuri wanaweza kushuka nafasi za chini kama hawatajitahidi katika baadhi ya michezo yao ijayo.
Takwimu za michezo mitano iliyopita zinaonesha kwamba hawakushinda mchezo hata mmoja zaidi ya kuambulia vipigo vitatu na sare mbili.
Wanahitaji kujirekebisha hasa safu yao ya ulinzi la sivyo kazi itakuwa kubwa mbele yao ambako ni kugumu kuliko walikotoka kwani kila timu inataka kuwa imara ili kuendelea kusalia kwenye ligi msimu ujao.
MBEYA CITY
Mbeya City ni timu iliyoanza kwa kasi msimu huu lakini kadiri siku zinavyokwenda inaporomoka. Kwa sasa iko katika nafasi ya tisa baada ya kucheza michezo 21 na kati ya hiyo kushinda michezo mitano, sare tisa na kupoteza michezo saba.
Katika michezo ya kemitano iliyopita pia haikuwa vizuri, imeshinda mchezo mmoja tu na mingine ikipoteza mitatu na kupata sare moja. Hii ilikuwa wiki ngumu kwa Mbeya City kwani walitoka kufungwa na Azam FC mabao 6-1, wakafungwa na Simba 3-2 na Tanzania Prisons 2-1.
Inaonesha ilikuwa wiki ya moto kwao ya vipigo na huenda imechangia kasi ya mabao ya kufungwa. Jumla ya mabao iliyofungwa katika michezo 21, ni 32 na imefunga mabao 27 kuonesha kuwa kwenye ulinzi kuna shida.
Bila shaka wanahitaji kasi ya kufunga lakini pia kuzuia na kuhakikisha wanafanya vizuri katika michezo yao ijayo ili kuepukana na hatari ya kushuka daraja.
POLISI TANZANIA
Maskini Polisi wanajikongoja kujiinua na kujiondoa hatarini. Huenda wakafanikiwa baada ya kufanya maboresho kwenye dirisha dogo la usajili. Lakini ni miongoni mwa timu zilizoanza vibaya msimu huu hadi kufikia hatua ya kubadilisha makocha na wachezaji.
Polisi ilikuwa inashika mkia na sasa imeanza kupanda hadi nafasi ya 15 ikitoka ya 16 baada ya kucheza michezo 21 na kati ya hiyo, kushinda mitatu, sare sita na kupoteza michezo 12. Ni miongoni mwa timu sita zinazoongoza kwa kupoteza michezo mingi.
Timu zote zilizoko chini kuanzia nafasi ya 11 hadi ya 16 kwa maana ya Ihefu, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, Coastal Union, Polisi yenyewe na Ruvu Shooting ndio timu zilizopoteza
michezo kuanzia 10 na kuendelea.
Polisi imefunga mabao 17 na imefungwa mabao 32 ikiwa na pointi 15 ambazo kiuhalisia haziwatoshi kujivunia au kuwapa nafasi ya kubaki salama kama wataendelea kufanya vibaya.
Lakini pengine, mwenendo wao hivi karibuni ni kama unaleta matumaini kwani michezo mitano waliyocheza inaonesha wameanza kubadilika. Katika idadi hiyo ya michezo ya karibuni wameshinda mmoja, wamepata sare tatu na kupoteza mmoja. Wanahitaji kupambana na lolote linawezekana kwao.
TANZANIA PRISONS
Hii ni moja ya timu ngumu hasa zinapokutana na vigogo hucheza soka la kiwango cha juu.
Lakini kama ilivyo kwa timu nyingine ndogo zikikutana zinazolingana kiwango huonekana wa kawaida.
Hawa walionekana kuanza vizuri na wanakoelekea wanaweza kumaliza vibaya kama wasipokuwa makini. Wanashika nafasi ya 12 kwa pointi 21 baada ya kucheza michezo 21, kushinda mitano, sare sita na kupoteza michezo 10.
Prisons imefunga mabao 18 na kufungwa 30 katika nyavu zao ikionesha kwenye ulinzi kama zilivyo nyingine hapo juu nao hawako vizuri.
Katika michezo mitano iliyopita, kuna mitatu ya karibuni iliyofungwa mabao mengi ukiwemo mchezo dhidi ya Simba walifungwa 7-1, wakapigwa na Azam FC 3-0 kisha na Ihefu 2-1.
Pia walishinda michezo mingine miwili dhidi ya Mbeya City mabao 2-1 na dhidi ya Dodoma Jiji 2-0.