Flamengo ‘kujilipua’ mbele ya Chelsea

PHILADELPHIA, Kocha wa klabu ya Flamengo ya Brazil Filipe Luis ameapa kuwa timu yake haitabadili mtindo wa uchezaji watakapoikabili Chelsea leo usiku akisema kwamba timu yake itasalia katika mtindo wao mkali na usio na huruma katika mtanange wa Kombe la Dunia la Klabu utakaopigwa katika dimba la Lincoln Financial Field mjini Philadelphia kuanzia saa 3 usiku saa za Afrika mashariki.
Flamengo, ambao wanaongoza ligi kuu ya Brazil watakuwa na kibarua Kizito cha kuendeleza matokeo mazuri waliyoanza nayo dhidi ya moja ya timu tishio kutoka bara la Ulaya huku wakiwa na hamasa ya kushinda mechi tano mfululizo katika michuano yote, ikiwa ni pamoja na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Esperance de Tunis katika mechi yao ya kwanza ya michuano hiyo.
Filipe Luis amesisitiza mbele ya waandishi wa Habari kuwa ujasiri na imani yake isiyoyumba katika falsafa ya timu yake ni silaha muhimu ya kiangamiza Chelsea ambayo kwa mujibu wake inachechemea.
“Kamwe usikate tamaa kwenye imani yako. Nina imani, wazo wazi la kile ninachofikiria kuhusu mchezo, Sitawahi kubadilisha timu yangu kwa sababu ya mpinzani. Itakuwa vibaya kabisa kwa wachezaji. Tutacheza jinsi tumekuwa tukijiandaa kwa miezi minane.” -Luis aliwaambia waandishi wa habari.
Filipe Luis amekitengeneza kikosi cha Flamengo ambacho kinaenjoy kumiliki mpira na kuamua kasi ya mechi. Hata hivyo, alikiri kwamba mechi dhidi ya Chelsea itahitaji “kujitolea” na akasisitiza umuhimu wa safu yake ya ulinzi yenye uzoefu wa beki wa zamani wa Juventus Danilo na Alex Sandro dhidi ya ubora wa timu hiyo ya Premier League.
Flamengo wanaongoza Kundi D wakiwa na pointi tatu sawa na Chelsea lakini wako kileleni kutokana na kigezo cha kadi za njano. Los Angeles FC na Esperance bado hawana pointi na watakutana katika mechi nyingine ya kundi hilo saa 7 usiku wa kuamkia Jumamosi.