Kwingineko

Eriksen aamua kupumzika baada ya kutoka hospitali

DENMARK: KIUNGO nyota wa Denmark, Christian Eriksen, ameondoa hofu kwa mashabiki wa soka duniani baada ya kuthibitisha kuwa anaendelea vizuri akiwa nyumbani pamoja na familia yake kufuatia kuanguka ghafla wakati wa mechi ya kirafiki kati ya Denmark na Ukraine wiki iliyopita.

Eriksen, mwenye umri wa miaka 34, alisema tukio hilo lilikuwa tofauti na lile la mwaka 2021 ambapo alipata mshtuko wa moyo akiwa katika mchezo wa Euro 2020 dhidi ya Finland.
Nyota huyo alieleza kuwa kifaa chake cha kusaidia mapigo ya moyo (ICD) kilifanya kazi kama kilivyokusudiwa kwa kutoa mshtuko wa umeme uliookoa hali yake wakati wa tukio hilo.

“Nataka kila mtu afahamu kwamba niko salama na ninaendelea vizuri nyumbani pamoja na familia yangu. Kama mnavyoweza kufikiria, kupokea mshtuko kutoka kwenye kifaa changu cha ICD kulikuwa jambo kubwa kwangu na kwa familia yangu, lakini nataka kuwahakikishia watu kuwa hali hii ilikuwa tofauti na ile ya mwaka 2021.

Najisikia vizuri na tayari nimeanza safari ya kupona,” alisema Eriksen.

Kiungo huyo wa zamani wa Manchester United na Brentford aliwashukuru wachezaji wenzake, madaktari wa uwanjani pamoja na wataalamu wa afya ambao wamekuwa wakimsimamia tangu alipopata tatizo kubwa la moyo miaka mitano iliyopita.

Alisema kwa sasa kipaumbele chake kikubwa ni kuendelea kupona na kutumia muda mwingi na familia yake kabla ya kufanya maamuzi kuhusu kurejea kwenye shughuli za soka la ushindani.

“Nitachukua muda wa mapumziko, kwenda likizo na kufurahia kucheza mpira na watoto wangu kabla ya kufikiria hatua inayofuata kuhusu maisha yangu ya soka,” aliongeza.

Tukio la hivi karibuni limerudisha kumbukumbu za siku ya Juni 12, 2021, wakati Eriksen alipoanguka ghafla katika mchezo wa Euro 2020 dhidi ya Finland mjini Copenhagen. Wakati huo, alikumbwa na mshtuko wa moyo na kupoteza fahamu uwanjani, hali iliyosababisha madaktari kufanya huduma za dharura za CPR kwa takribani dakika 10 huku wachezaji wakimzunguka kumlinda dhidi ya macho ya umma.

Baadaye alipelekwa hospitalini akiwa ametulia na ndipo madaktari walipomfungia kifaa cha ICD, teknolojia iliyomwezesha kurejea tena kucheza soka la kulipwa mwaka 2022.

Karibu miaka mitano baadaye, Juni 6, 2026, Eriksen alianguka tena wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Ukraine. Tofauti na tukio la awali, safari hii alikuwa bado na fahamu wakati wa tukio hilo, ingawa mchezo ulisitishwa mara moja kutokana na hali hiyo.

Tangu kurejea kwake uwanjani baada ya tukio la mwaka 2021, Eriksen amekuwa mfano wa uthabiti na mapambano dhidi ya changamoto za kiafya, huku akifanikiwa kurejea katika kiwango cha juu cha soka la kimataifa na klabu.

Kwa sasa, mashabiki wa Denmark na dunia nzima wanaendelea kufuatilia maendeleo yake huku wakitumaini kumuona nyota huyo akirejea tena uwanjani baada ya kukamilisha mchakato wake wa kupona.

Related Articles

Back to top button