Kwingineko

Slot: ilikuwa mechi bora sana

LIVERPOOL:BOSI wa majogoo wa jiji, Arne Slot, ameutaja mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya PSG jana Jumanne kama mchezo bora zaidi wa mpira wa miguu kuwahi kuusimamia kama kocha, licha ya kikosi chake kutupwa nje ya michuano hiyo kwa mikwaju ya penalti.

Liverpool walikuwa wa kwanza kuwaonjesha joto la jiwe PSG kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza kwa ushindi wa 1-0 dakika za jioni kwenye dimba la Parc des Princes, kisha PSG kulipiza kisasi Anfield jana kwa bao la Ousmane Dembele dakika ya 12.

Akizungumza na Amazon Prime baada ya mchezo huo, Slot amesema mchezo huo ulikuwa bora zaidi kwake kuusimamia kama meneja na licha ya kushindwa kupenya hatua hiyo, bado anaamini ana kikosi bora na walicheza vizuri sana.

“Ulikuwa mchezo bora zaidi wa mpira wa miguu kwangu kuwahi kuusimamia. Tulicheza vizuri sana ukilinganisha na mchezo uliopita, najivunia hilo. Labda hatukuwa na bahati tu. Kikosi changu kilicheza vizuri. Tulifanya kama wao tu kule Paris walicheza vizuri lakini hawakupata bao.”

Liverpool walitengeneza nafasi nyingi za kufunga bao lakini hawakuzitumia, kupelekea mchezo huo kwenda dakika 30 za nyongeza na kuamuliwa kwa mikwaju ya penati, iliyompa ujiko golikipa wa PSG, Gianluigi Donnarumma, aliyechomoa mikwaju ya Darwin Nunez na Curtis Jones, muda mchache baada ya Mohamed Salah kuweka moja kambani, hivyo ubao wa penati kusoma 4-1.

Baada ya kuondoshwa kwenye UCL, Liverpool sasa wana makombe mawili ya ndani ya kushindania, ikiwa ni Carabao Cup wakiwa fainali dhidi ya Newcastle na Ligi Kuu ya Nyumbani kwao wanayoshikilia usukani kwa tofauti ya pointi 15.

Related Articles

Back to top button