Unai Emery: Sijawahi ona kosa kama lile maishani mwangu!
KOCHA mkuu wa Aston Villa Unai Emery amesema kosa alilofanya beki wake wa kati Tyrone Mings dakika ya 50 ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya dhidi ya Club Brugge ni la ajabu na hajawahi kuona kosa kama lile katika maisha yake ya Soka.
Mings aliyerejea uwanjani baada ya kuwa nje ya kwa takriban miezi 14 kutokana na jeraha la goti aliadhibiwa baada ya kuokota mpira uliotoka kwa golikipa wake Emiliano Martinez katika eneo lao la 18 jambo lililomlazimu mwamuzi wa mchezo huo Tobias Stieler kuwapa penalty wapinzani wao Club Brugge na Hans Vanaken kuweka kambani bao pekee la mchezo lililositisha mwendo mzuri wa klabu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Akizungumza baada ya mchezo huo Unai Emery hakumtupia lawama mwamuzi wa mchezo huo licha ya kuonekana akiwa katika majadiliano mazito mara kadhaa na mwamuzi wa akiba wa mchezo huo.
“Tumecheza vizuri kipindi cha kwanza, kosa la kipindi cha pili lilibadilisha kila kitu kibaya zaidi ni kosa tulilofanya. Lilikuwa jambo la ajabu mno, nadhani limetokea mara moja tu maishani mwangu, sijawahi ona kosa kama lile” – Amesema kocha huyo.
Aston Villa wamekuwa na mwanzo mzuri kwenye ligi hiyo wakishinda mechi 3 ikiwemo mechi dhidi ya mabingwa wa zamani wa Ligi hiyo, Bayern Munich kisha kushinda dhidi ya Celtic na Bologna kabla ya kupoteza hapo jana dhidi ya Club Brugge ugenini katika dimba la Jan Breydelstadion uliofurika mashabiki zaidi ya 23 elfu.