Masumbwi

Dulla Mbabe nusura azichape kavukavu

DAR ES SALAAM:BONDIA wa ngumi za kulipwa Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ nusura azichape kavukavu na bondia kutoka Zambia Mbachi Konga wakati wa kutambulisha pambano la Knockout ya Mama.

Katika tukio hilo lililofanyika Dar es Salaam jana kwenye viwanja vya Magomeni Sokoni chini ya Mafia Promotion, Dulla Mbabe alionesha kumvimbia mpinzani wake na kuanza kumchokoza kwa kutaka kulianzisha na mpinzani wake alijipibu mapigo.

Kama sio walinzi kuingilia kati ingekuwa ni habari nyingine lakini mwisho wa siku wote walitambiana kila mmoja atamuonesha mwenzake ngumi zinavyochezwa.

Chanzo kilianzia kwenye maneno yao ya tambo ambapo Dulla alisema:”Huyu hapa ni sawa na babu katoka ndani badala ya kuchukua ‘boxer’ kachukua sidiria ya bibi katoka nayo kaingia choo cha kiume, ukiingia choo cha kiume lazima ujikojolee huko huko, hawezi kutoka mimi nitaishi naye”.

Kwa upande wa Konga alijibu hivi: “Sijacheza ngumi kwa muda mrefu lakini kesho (leo) utaishuhudia ngumi yangu ya hatari, nitakwenda kukufundisha namna ya kucheza ngumi, wewe hujui lolote,”
Maneno hayo yalimtia hasira Dulla na kupandisha mori kiasi cha ghafla kumvamia mpinzani wake na kumwambia anazungumza sana.

Hao ni miongoni mwa mabondia watakaopanda ulingoni leo usiku katika pambano la Knockout ya Mama Magomeni Sokoni kusindikiza pambano kuu la mtoto wa bondia wa zamani Rashid Matumla ‘Snake boy’ Amir Matumla dhidi ya bondia wa Namibia Paulus Amavila.

Mapambano mengine yatakayochezwa leo ni Kalolo Amiry dhidi ya Mussa Kananji, Said Chino dhidi ya Gael Assumani wa DR Congo, Oscar Richard dhidi ya Bongani Makovora, Dulla Mbabe dhidi ya Mbachi Konga wa Zambia na Haidary Mchanjo dhidi ya George Bunabucha.
Mapambano hayo yanatarajiwa kushuhudiwa na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.

Related Articles

Back to top button