Tanzania mabegani mwa King Lucas Mwajobaga leo

TUNIS: BONDIA wa Timu ya Taifa ya Ngumi maarufu kama Faru Weusi wa Ngorongoro King Lucas Mwajobaga atapanda ulingoni usiku wa leo kupeperusha bendera ya Tanzania dhidi ya Liduema Elder kutoka Angola katika mapambano ya kwanza ya semi-pro ya usiku wa Solidarty & Fratenity Boxing Gala katika mji wa Tunis, Tunisia.
Pambano hilo la round 6 katika uzani wa 63.5 ni la kwanza Kimataifa nje ya Tanzania kwa King Lucas na ameahidi kufanya makubwa na kuliheshimisha Taifa katika ardhi ya Tunisia.
King Lucas ameambatana na Mwalimu Mkuu wa Timu ya Taifa Samwel Kapungu na Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) Lukelo Willilo ambapo mapambano 10 yatapigawa usiku wa leo kuanzia majira ya saa 2 usiku.
Mapambano hayo mapya ya semi-pro ya IBA na AFBC yameandaliwa na wenyeji chama cha Ngumi cha Tunisia huku toleo la pili likitarajiwa kufanyika nchini Tanzania mwisho wa mwezi February 2025.