Mchanja kuwania mkanda wa WBO

DAR ES SALAAM: BONDIA Yohana Mchanja ‘Komputa’ ameahidi kufanya vizuri katika pambano la mkanda wa kimataifa wa WBO dhidi ya bondia kutoka Ufilipino Miel Fajardo litakalopigwa Desemba 26, mwaka huu Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam leo Mchanja amesema amejipanga vizuri anasubiri siku hiyo ngumi ziongee kwa vitendo.
“Lengo langu ni kubakiza mkanda nyumbani, nimejipanga vizuri namuahidi Rais Samia Suluhu Hassan kumpa mkanda,”amesema.
Mtendaji Mkuu wa Mafia Boxing Promotions Ally Zayumba amesema pambano hilo linaloitwa ‘Knockout’ ya mama litakutanisha mapambano 13 kwa mabondia wa ndani nan je ya nchi.
Amesema wamewaandaa mabondia wa Tanzania kwa kuwapeleka kambi ya Afrika Kusini kujiweka imara ambapo tayari wamerudi wanamalizia mazoezi ya mwisho nyumbani.
Zayumba amesema lengo ni kuhakikisha mabondia hao sio tu wanashiriki bali wanashinda mikanda hiyo mikubwa.
Mabondia wengine watakaowania mikanda mikubwa ni Ibrahim Mafia dhidi ya Lusinzo Mazana wa Afrika Kusini mkanda wa WBC Afrika, Salmin Mizinga dhidi ya Adrian Lerasan wa Ufilipino mkanda wa WBF, Said Chino dhidi ya Malcom Classen wa Afrika Kusini mkanda wa IBA Afrika.
Wengine watakaochuana ni Mfaume Mfaume dhidi ya Amavila Paulus wa Namibia, Said Bwanga dhidi ya Guprity Singh wa India, Salmin Mtango dhidi ya Azeed Latif wa Nigeria.