BSS yalamba donge nono

DAR ES SALAAM: BENKI ya CRDB imedhamini rasmi mashindano maarufu ya kusaka vipaji nchini, Bongo Star Search 2026, ambayo sasa yatakuwa yakifahamika kama CRDB Bank Bongo Star Search 2026.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya CRDB Bank, Palm Beach jijini Dar es Salaam, Madam Rita amesema ujio wa benki hiyo kwenye mashindano hayo ni hatua kubwa inayodhihirisha namna taasisi kubwa zinavyoendelea kuthamini na kuwekeza kwenye vipaji vya vijana wa Kitanzania.
“Kama mnavyojua, ujio wa CRDB Bank msimu huu umeongeza mambo mengi makubwa kwenye mashindano haya,” amesema Madam Rita.
Ameeleza kuwa msimu wa mwaka 2026 utakuwa na maboresho mbalimbali ikiwemo kuongezwa kwa vipengele vya sarakasi, uchoraji pamoja na wachekeshaji, huku washiriki wakipata pia elimu ya fedha kupitia wataalamu kutoka CRDB Bank.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa CRDB Bank, Stephen Adili, amesema kupitia jukwaa la ‘Konekt na CRDB’ chini ya huduma za kibenki kwa vijana, benki hiyo imelenga kuwawezesha vijana kufikia ndoto zao kupitia vipaji.
“Maisha ya vijana ndiyo kipaumbele kikubwa, na hilo ndilo litakalotekelezwa kupitia CRDB Bank Bongo Star Search 2026,” amesema Adili.
Mkutano huo umehudhuriwa na jopo la majaji wa mashindano hayo akiwemo Madam Rita ambaye pia ni mkurugenzi wa BSS, pamoja na Master Jay na Coy Mzungu.




