BurudaniFilamu

HARD TARGET

NDANI ya mitaa ya jiji la New Orleans nchini Marekani, Douglas Binder hakuijua kula yake kama ilivyo kwa masikini wengine wa eneo hilo.

Anayakubali hayo na kuyaishi maisha yake. Pamoja na hali yake ya kukosa mahitaji muhimu hakuwahi kumwibia mtu yeyote, na anawasaidia wenzake wanaohitaji.

Hadi inapokuja siku ya leo, siku ngumu kwake, siku anayopewa mkanda wenye dola 10,000
za Marekani na kutakiwa aufunge kiunoni na akimbie kadri ya uwezo wake.

Anaambiwa kuwa akifanikiwa kufika upande wa pili wa mji salama basi fedha hiyo ni yake. Hii haikuwa hiari, ilikuwa ni lazima afanye hivyo. Huu ni mchezo wa kishenzi unaochezwa na washenzi tu wenye fedha ambao kazi yao ni kuchezea kamari maisha ya watu.

Ukijidhani kwamba unafaa kukimbia jua unakosea, kwani huu ni mchezo wa kuwindwa
(hunting) kama mnyama. Ili kuipata fedha hiyo inabidi uwindwe kwa kila aina ya silaha nzito yenye kutoa uhai wa watu.

Douglas Binder anavaa mkanda huo kiunoni na kuanza safari ya kukatisha mji hadi upande wa pili. Ni hivyo tu! Anakimbia mwanzo lakini anashindwa mwisho. Kwenye daraja la mbao katikati ya mto, Douglas anapigwa mshale wa umbali mrefu na kushindwa kumaliza safari yake, anauawa na safari inaishia hapo.

Van Cleef, kiongozi wa wawindaji anamfumba macho kwa kiatu na kuchukua fedha zao, kisha wanaondoka. Kitabu cha maisha ya Douglas kinafungwa rasmi. Natasha, binti wa Douglas Binder, anarudi kutoka masomoni akiamini kuwa atamkuta baba yake.

Kila anapofika kuulizia anaambiwa kuwa Douglass hajaonekana. Pilika pilika za siku nzima za kumtafuta mzee wake zinamchosha na hivyo anaamua kwenda kwenye mgahawa ndani ya eneo dogo la Hermagodo.

Muda wote huo Natasha hakuwa akijua chochote kuhusu maisha ya watu wa eneo lile. Anatoa fedha na kuhudumiwa kisha anatoka. Ni mtu mmoja tu anayeitwa Chance Boudreaux ndiye anajua kuwa Natasha anafanya kosa kubwa sana kuonesha fedha nyingi hadharani katika eneo hilo.

Boudreaux ni mmoja wa watu wasio na makazi lakini ni fundi wa sanaa ya mapigano,
bingwa wa mateke ya uzani wa juu duniani anayei shi eneo hilo. Ndani ya eneo lile wahuni
wanaosubiri kumdhuru mtu yeyote mwenye fedha ni wengi kuliko maduka yanayouza
bidhaa.

Kwa kuuelewa mchezo mzima, Boudreaux anatangulia kutoka ili Natasha akitoka aweze kumsaidia endapo wahuni hao wakitaka kumpora. Na kama alivyowaza ndivyo inavyotokea.

Natasha anapotoka tu nje ya mgahawa anakutana na asichokijua wala kukitarajia wakati wahuni wanapomvamia wakitaka kuchukua mkoba wake wenye fedha nyingi. Akiwa katika tahayari ndipo anajitokeza mtu mwingine asiyemjua (Boudreaux) pia.

Boudreaux anawahesabu wale wahuni kwa macho kisha anafunua koti mguu wake wa kulia. Mguu mmoja unabaki chini na ule mwingine unasafiri juu bila kutua chini kwenye vichwa vya wahuni watatu kwa kasi ya ajabu.

Natasha haamini kinachoendelea eneo hilo. Ndani ya dakika mbili anajikuta akizubaa asijue
kinachotokea. Anawaza; inawezekana vipi binadamu akawa mwepesi kiasi kile! Muda anaomaliza kuwaza anakuta tayari Boudreaux ameshawaweka watu watano chini.

Natasha anamhusudu Boudreaux na kumwomba awe mlinzi wake na amsaidie kumtafuta
baba yake. Ni hapo kizaazaa kinapoanzia. Fisi anakabidhiwa bucha alinde! Natasha anamuahidi mhuni Boudreaux fedha nyingi.

Boudreaux hakutaka kujiingiza kwenye misheni za Natasha lakini anaahidi kumsaidia.
Mpelelezi wa polisi wa New Orleans, Marie Mitchell anasita kufanya uchunguzi wa kutoweka kwa Douglas Binder hadi mwili wake uliochomwa unapopatikana katika majivu ndani ya jengo lililotelekezwa.

Ni katika kutafuta kwake ukweli wa kilichomtokea Douglas Binder, baba wa Natasha, Boudreaux anajikuta akihesabiwa na kikosi cha Van Cleef kama windo jipya. Wawindaji wanapoona Boudreaux anakaribia kuujua ukweli wa kilimchotokea Douglas, wanaamua kumwangamiza yeye na Natasha.

Wasichojua ni kwamba wamefanya kosa kubwa. Van Cleef anaamini kuwa Boudreaux wala hahitaji kupewa mkanda wa fedha afunge kiunoni. Wanaamini kuwa itakuwa ni kazi rahisi
kama wanavyowafanya wengine siku zote. Hilo linakuwa kosa jingine kubwa.

Boudreaux hakamatiki kirahisi, kikosi cha Van Cleef hawajui kuwa Boudreaux ni askari wa zamani wa kikosi maalumu cha jeshi (Force Recon Marine). Kama ni vita basi inamtambua Boudreaux ni nani.

Boudreaux anamwambia Natasha, “niamini, hapa upo kwenye mikono salama ya mwanajeshi”. Natasha anavua mkoba wake, anaweka bega lake kwenye kifua cha Boudreaux na kumkabidhi maisha yake.

Boudreaux anaacha alama ya nyayo kuwaonesha adui alipoelekea akiamini watamfuata. Ni kweli wanamfata na wanamkuta akiwa kauvaa ujasiri wake wa kipindi kirefu. Van Cleef na kikosi chake wanaandaa silaha zote za moto na za jadi.

Boudreaux anafunga kitambaa mkononi na kuwakaribisha kwenye uwanja wake wa  nyumbani. Ni mwendo wa aksheni za nguvu na ufundi wa kumpunguza mmoja mmoja hadi pale Van Cleef anapogundua kuwa watu wake wanapungua, anaamua kumwita Boudreaux.

Anamuuliza, “kwani wewe ni nani!” Muda ambao Van Cleef hamjui Boudreaux jina ndiyo
muda ambao Boudreaux anavua shati na kubaki na singlendi. Baada ya kuona wameshindwa, adui hao wanataka amani wakati Boudreaux ndiyo kwanza anaanza
vita.

Hawakujua kwamba wameingia choo cha kike. Hard Target ni filamu iliyotoka mwaka 1993 nchini Marekani, ni filamu yenye aksheni za nguvu ikiwa imeongozwa na mwongozaji wa Hong Kong, John Woo, na imemshirikisha nyota wa filamu za mapigano, Jean-Claude Van Damme ambaye amecheza kama Chance Boudreaux.

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

Related Articles

Back to top button