Bollywood yampoteza muongoza filamu Kuku Kohli

MUMBAI: DUNIA ya filamu ya Bollywood imeendelea kuomboleza kifo cha mtayarishaji na muongozaji mkongwe wa filamu, Kuku Kohli, huku mazishi yake yaliyofanyika jijini Mumbai Jumatano, Agosti 26, 2026, yakihudhuriwa na mastaa mbalimbali wa tasnia hiyo.
Kuku Kohli alifariki Jumanne, Agosti 25, 2026, akiwa na umri wa miaka 77, baada ya kupata mshtuko mkubwa wa moyo akiwa katika Hospitali ya Kokilaben Dhirubhai Ambani mjini Mumbai.
Taarifa za kifo chake zilithibitishwa na watu waliokuwa karibu naye pamoja na vyombo mbalimbali vya habari vya India.
Mazishi yake yalifanyika Oshiwara Crematorium jijini Mumbai, ambapo watu mbalimbali kutoka sekta ya filamu walifika kutoa heshima zao za mwisho.
Miongoni mwa mastaa waliohudhuria ni Katrina Kaif, Vicky Kaushal, Rohit Shetty, Javed Akhtar, Shabana Azmi, Raza Murad na Tinu Anand.
Mke wa marehemu, mwigizaji mkongwe Aruna Irani, alionekana akiwa mwenye huzuni kubwa wakati wa kuaga mwili wa mumewe, huku picha na video kutoka kwenye mazishi hayo zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Kuku Kohli anakumbukwa zaidi kwa kuiongoza filamu ‘Phool Aur Kaante’, iliyotoka mwaka 1991 na kumpa Ajay Devgn nafasi iliyosaidia kuanza safari yake kubwa katika tasnia ya Bollywood.
Kifo cha Kohli kimemgusa pia Ajay Devgn, ambaye ametoa heshima zake kwa mkurugenzi huyo akimshukuru kwa kumuamini na kumpa nafasi katika filamu hiyo iliyokuwa mwanzo muhimu wa safari yake ya uigizaji.
Mbali na ‘Phool Aur Kaante’, Kohli alihusika katika filamu kadhaa za Bollywood, zikiwemo ‘Suhaag’, ‘Haqeeqat’, ‘Anaari No. 1’ na ‘Zulmi’, na ameacha historia ya zaidi ya miongo mitatu katika sinema za India.




