Bundesliga

Nkunku arejea RB Leipzig kwa mkopo kutoka AC Milan

LEIPZIG: Mshambuliaji wa Ufaransa, Christopher Nkunku, amerejea katika klabu yake ya zamani ya RB Leipzig baada ya klabu hiyo ya Bundesliga kumsajili kwa mkopo wa msimu mmoja kutoka AC Milan, huku ikiwa na chaguo la kumnunua moja kwa moja.

Uhamisho huo ulithibitishwa rasmi na RB Leipzig na AC Milan, kabla ya taarifa hiyo kuendelea kuripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari Jumatano, Agosti 26.

Kwa mujibu wa AC Milan, Nkunku amejiunga na Leipzig kwa mkopo hadi Juni 30, 2027, huku klabu hiyo ya Ujerumani ikiwa na haki ya kufanya uhamisho huo kuwa wa kudumu.

Nkunku, mwenye umri wa miaka 28, aliwahi kuitumikia RB Leipzig kati ya mwaka 2019 na 2023, kipindi ambacho alifanya vizuri na kuwa miongoni mwa washambuliaji hatari katika Bundesliga.

Katika kipindi chake cha kwanza Leipzig, Nkunku alicheza jumla ya michezo 172, akifunga mabao 70 na kutoa pasi za mabao 56, huku akisaidia klabu hiyo kushinda mataji mawili ya Kombe la Ujerumani.

Baada ya kuondoka Leipzig mwaka 2023, alijiunga na Chelsea, kabla ya kuhamia AC Milan. Hata hivyo, msimu wake mmoja nchini Italia haukuwa na mafanikio makubwa kama ilivyotarajiwa, kwani alifunga mabao 8 katika michezo 35 kwa AC Milan.

Baada ya kukamilika kwa uhamisho huo, Nkunku amesema alikuwa na hamu kubwa ya kurejea Leipzig mara tu nafasi hiyo ilipojitokeza.

Mchezaji huyo amesema uhusiano wake na RB Leipzig ni wa kipekee na yuko tayari kuanza ukurasa mpya katika klabu hiyo.

“Nina furaha sana kurudi. Niko katika hali nzuri na nataka kuisaidia timu mara moja. Siwezi kusubiri kucheza tena mbele ya mashabiki wetu katika Red Bull Arena,” alisema Nkunku.

Mkurugenzi wa michezo wa RB Leipzig, Marcel Schäfer, amesema klabu hiyo imefurahishwa na kurejea kwa Nkunku, akisisitiza kuwa mchezaji huyo anaifahamu vizuri klabu, jiji na mazingira yake.

Related Articles

Back to top button