Sterling kufikishwa Mahakamani

LONDON: NYOTA wa zamani wa England na Manchester City, Raheem Sterling, atafikishwa mahakamani mwezi ujao baada ya kushtakiwa kwa makosa ya kuendesha gari kwa hatari na matumizi yasiyo sahihi ya gesi ya nitrous oxide.
Sterling, 31, anatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Basingstoke Magistrates, England, Septemba 15, 2026, kufuatia ajali iliyohusisha gari lake aina ya Lamborghini katika barabara ya M3, Hampshire, Mei 28 mwaka huu.
Kwa mujibu wa polisi, Sterling anadaiwa kuendesha gari kwa hatari, kumiliki nitrous oxide kwa matumizi yasiyo sahihi na kushindwa kutoa sampuli iliyohitajika.
Ajali hiyo ilihusisha gari moja pekee na hakuna mtu aliyejeruhiwa, huku Sterling akikamatwa baada ya tukio hilo na baadaye kuachiwa kwa dhamana wakati uchunguzi ukiendelea.
Awali polisi walikuwa wakimchunguza kwa tuhuma za kuendesha gari akiwa katika hali isiyofaa kutokana na matumizi ya dawa, lakini shtaka hilo halijawekwa kwenye mashtaka yaliyotangazwa.
Sterling kwa sasa hana klabu baada ya kumaliza mkataba wake mfupi na Feyenoord ya Uholanzi, aliyojiunga nayo Februari baada ya kuondoka Chelsea kwa makubaliano ya pande zote.
Mshambuliaji huyo alitengeneza jina kubwa akiwa Manchester City, ambako alishinda mataji manne ya Ligi Kuu England, Kombe la FA na Kombe la Ligi mara tano.
Pia aliwahi kuichezea Liverpool na Arsenal kwa mkopo, huku akicheza mechi 82 kwa timu ya taifa ya England kati ya mwaka 2012 na 2022.
Sasa, mbali na changamoto ya kutafuta klabu mpya, Sterling anakabiliwa na mtihani mwingine nje ya uwanja, huku kesi yake ikitarajiwa kuanza Septemba.




