Bao la Ronaldo dhidi ya Croatia laandika historia mpya Kombe la Dunia

TORONTO:BAO alilofunga Cristiano Ronaldo kwenye ushindi wa mabao 2-1 wa Ureno dhidi ya Croatia limeandika historia mpya katika Kombe la Dunia 2026.
Hilo lilikuwa bao la kwanza kabisa kwa Ronaldo kufunga katika hatua za mtoano za Kombe la Dunia tangu aanze kushiriki mashindano hayo, rekodi ambayo alikuwa hajawahi kuifikia katika michuano yake yote iliyopita.
Bao hilo pia limemfanya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kufunga katika hatua za mtoano za Kombe la Dunia akiwa na miaka 41 na siku 147.

Mbali na rekodi hiyo, Ronaldo ameweka historia nyingine kwa kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kucheza mechi ya hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia.
Nahodha huyo wa Ureno aliisaidia timu yake kutinga hatua inayofuata huku akiendelea kuongeza rekodi mpya katika historia ya soka duniani.
Licha ya umri wake wa miaka 41, Ronaldo ameendelea kuthibitisha kuwa bado ni mchezaji wa kuamua mechi kubwa na mmoja wa magwiji wakubwa kuwahi kutokea kwenye mchezo wa soka.
Katika hatua inayofuata, Ureno itacheza na Hispania kutafuta mshindi atakayeingia robo fainali.



