Singida yapania kuwapa somo Tusker

DAR ES SALAAM: SINGIDA Black Stars imeweka wazi kuwa iko tayari kwa kibarua kinachofuata dhidi ya Tusker ya Kenya katika Kombe la Shirikisho Afrika, ikisema mchezo huo utakuwa zaidi ya kusaka tiketi ya hatua ya makundi kutokana na ushindani wa Tanzania na Kenya.
Baada ya kuanza kampeni hiyo kwa ushindi wa mabao 10 dhidi ya Al Ghazala, Singida sasa imehamishia nguvu zake Tusker, huku ikiamini ubora wa kikosi chake unaweza kuwa silaha muhimu katika kuikabili timu hiyo ya Kenya.
“Tumebaki mchezo mmoja tu kwenda hatua ya makundi, kwa hiyo tuna mechi dhidi ya Tusker. Upekee wa mchezo huu si ubora wa timu hizi mbili, bali ni nchi hizi mbili kukutana,” amesema Ofisa Habari wa Singida Hussein Masanza.
Amesema Singida ina kikosi chenye ubora wa kutosha, kuanzia kwenye profaili za wachezaji hadi benchi la ufundi, hivyo hawana sababu ya kuwa na hofu wanapokutana na Tusker.
Hata hivyo, amesema historia ya michezo kati ya Tanzania na Kenya imekuwa ikifanya mechi za aina hiyo kuwa na ushindani mkubwa, kwa kuwa nchi hizo ni majirani na kila upande hutaka kuonesha ubora wake.
“Tunawafahamu Wakenya ni watu wa maneno mengi. Wanatuona Watanzania kama wanatuweza sana, lakini ubora ambao tutaenda kuonesha kwenye mchezo huu utaenda kutoa somo kubwa kwa Wakenya kwamba Tanzania imeshaacha mbali sana katika mpira wa miguu,” amesema.




