Afrika Mashariki

Ujumbe wa Akothee kwa Omondi kifo cha Fred Omondi

NAIROBI, Kenya: MSANII na mjasiriamali Esther Akoth, almaarufu Akothee, amemwandikia mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi ujumbe wa faraja leo Jumamosi, Juni 29 wakati wa mazishi ya mdogo wake Fred Omondi.

Fred Omondi, ambaye aliaga dunia wiki mbili zilizopita baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani wakati pikipiki aliyokuwa akiendesha ilipogongana ana kwa ana na matatu mapema asubuhi jijini Nairobi, amezikwa nyumbani kwao eneo la Sega, Kaunti ya Siaya.

Katika ujumbe wake kwa Eric, Akothee amemtaka awe na moyo wa kijasiri, akubali kwamba amempoteza ndugu yake, ni jambo linalouma lakini anatakiwa akubaliane nalo ingawa si rahisi kiasi hicho.

“Leo naomboleza na wewe ndugu yangu @ericomondi, kwa nje inaweza kuonekana imedhibitiwa, lakini ndani maumivu ni makubwa sana. Kupoteza mpendwa si rahisi, na kwa mtu aliyekua yatima naelewa undani wa kile unachopitia kwa sasa,” Akothee alimwandikia Eric.

Hata hivyo, Akothee alibainisha kuwa Eric atakuwa katika nafasi nzuri kwa sababu, mwisho wa siku, ana mtoto na mke wa kumfariji baada ya kumpoteza kaka yake pekee aliyesalia kufuatia kifo cha kaka yao mwingine mwaka 2018.

“Kaka weka kichwa juu. Niko pamoja nawe katika safari hii ya upweke. una mke na mtoto wa kukufariji. Familia iliyotoka kwako inaleta faraja na furaha kubwa. Huo ndio uamuzi bora zaidi uliowahi kufanya. Nakupenda, ndugu.

Rambirambi zangu za dhati na ndugu na rafiki yetu FRED OMONDI apumzike kwa amani,” Akothee alimalizia.
Ibada ya wafu ya Fred Omondi ilifanyika jana, Ijumaa, katika Hifadhi ya Maiti ya Chiromo, ambapo nyota kadhaa walihudhuria kumpa Eric Omondi faraja.

Baadaye, mwili wake ulisafirishwa kwa ndege kutoka Nairobi hadi Kisumu na kisha kusafirishwa kwa barabara hadi Siaya, ambapo amezikwa.

Related Articles

Back to top button