Muziki

Harmonize afichua ndoto yake ya soka ilivyokufa kabla ya muziki

DAR ES SALAAM: MSANII maarufu wa muziki Tanzania, Harmonize, amefichua kuwa muziki haukuwa ndoto yake ya kwanza, bali alikuwa akitamani kuwa mchezaji wa soka kabla ya mazingira ya maisha kumlazimisha kuachana na ndoto hiyo na kuingia rasmi kwenye muziki.

Harmonize alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika kipindi cha Obinna TV Extra nchini Kenya, akieleza kuwa wakati akiwa mwanafunzi wa sekondari, muda wake mwingi aliutumia kwenye uwanja wa mpira.

“Mimi nilikuwa mchezaji wa mpira wa shule, huo ndio ulikuwa kipaji changu cha kwanza kabisa,” alisema Harmonize.

Alieleza kuwa baada ya kumaliza shule alihamia Dar es Salaam kwa ajili ya kutafuta kazi, ambako aliishi kwa mume wa dada yake. Hata hivyo, majukumu ya kusaidia shughuli za familia yalimfanya ashindwe kupata muda wa kutosha wa kufanya mazoezi ya soka.

Kwa mujibu wa Harmonize, soka lilihitaji muda maalumu wa mazoezi, wakati yeye alilazimika pia kusaidia kazi katika duka la familia. Hatimaye, hali hiyo ilisababisha ndoto yake ya kuwa mchezaji wa kulipwa kufifia.

Baada ya kuachana na soka, Harmonize alianza kuupa muziki nafasi kubwa, akichochewa pia na watu waliokuwa wakimzunguka ndipo akaingia katika mashindano ya Bongo Star Search, kabla ya kusaini mkataba na WCB mwaka 2015 na hatimaye kuanzisha kampuni yake ya muziki, Konde Gang.

Leo, Harmonize ni miongoni mwa wasanii wanaotambulika katika muziki wa Bongo Flava, huku akifikisha takribani miaka 10 katika tasnia hiyo.

Msanii huyo pia amewataka wasanii chipukizi na wenye ndoto ya kufanikiwa kupitia muziki kutokata tamaa katika kufuatilia ndoto zao, akisisitiza kuwa mazingira ya maisha yasiwakatishe tamaa huku wakiendelea kupambania vipaji vyao.

Related Articles

Back to top button