Amber Ray afunguka upasuaji wa mwili wake Uturuki

NAIROBI: MWANAMITANDAO maarufu wa Kenya, Amber Ray, amefunguka kuhusu uamuzi wake wa kusafiri hadi Uturuki kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa mwili wake, akisema alichukua hatua hiyo kwa ajili ya kujipa furaha na kujiamini zaidi, si kwa ajili ya kumridhisha mtu mwingine.
Amber amesema anaamini mwanamke anatakiwa kujipenda mwenyewe kabla ya maoni ya watu wengine. Kupitia ujumbe wake, alisisitiza kuwa kauli yake ya “I Come First” (Mimi ndiye wa kwanza) ndiyo falsafa inayomuongoza katika kufanya maamuzi yanayohusu mwili na maisha yake binafsi.
Mrembo huyo alieleza kuwa alifanya maandalizi ya kutosha kabla ya kufanyiwa upasuaji huo nchini Uturuki, akiwemo kupata ushauri wa madaktari bingwa na kuhakikisha anachagua hospitali yenye viwango vya kimataifa. Alisema afya na usalama wake vilikuwa kipaumbele kikubwa katika mchakato mzima.
Amber pia aliwataka wanawake kutofanya maamuzi ya kubadili miili yao kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa wapenzi au mitandao ya kijamii. Badala yake, alisisitiza kuwa kila mtu anapaswa kufanya kile kinachomfanya ajisikie vizuri, mradi tu kinafanywa kwa usalama na kwa ridhaa yake mwenyewe.
Kauli zake zimezua mjadala mkubwa mitandaoni, huku baadhi ya watu wakimuunga mkono kwa kuthamini uhuru wa mtu binafsi juu ya mwili wake, na wengine wakionesha wasiwasi kuhusu ongezeko la watu wanaokimbilia upasuaji wa urembo. Licha ya maoni hayo tofauti, Amber amesema hana majuto na anaendelea kufurahia matokeo ya uamuzi wake.




