Nyumbani

T9 yaita wafanyabiashara AFCON 2027

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Habari na Mawasiliano ya T9 imesema Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa Tanzania, ikiwataka wafanyabiashara kuanza kujiandaa mapema ili kunufaika na mamilioni ya wageni watakaofika nchini wakati wa mashindano hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa T9, Othman Abdulrazak, amesema ushirikiano wa serikali za Tanzania, Kenya na Uganda katika maandalizi ya AFCON 2027 utafungua milango ya uwekezaji, biashara na ajira kwa Watanzania, hususan vijana.

Amesema wameandaa mfumo maalumu wa biashara utakaowawezesha wafanyabiashara kuunganishwa na fursa zitakazozalishwa na mashindano hayo, ikiwemo sekta za usafirishaji, malazi, utalii, huduma za kifedha, usambazaji wa bidhaa na teknolojia.

“AFCON ni jambo kubwa kwetu. Tukijiandaa kwa weledi, si tu tutanufaika kiuchumi, bali Tanzania itaonesha uwezo wake wa kuandaa matukio makubwa ya kimataifa na hivyo kuvutia wawekezaji zaidi pamoja na mashindano mengine makubwa,” amesema Othman.

Ameongeza kuwa T9 imejenga miundombinu ya kidijitali na mfumo wa biashara utakaorahisisha wafanyabiashara kunufaika na matumizi ya wageni watakaohudhuria michuano hiyo, huku akisisitiza kuwa tukio hilo litafungua ajira nyingi kwa vijana katika sekta mbalimbali.

Sambamba na hilo, kampuni hiyo imetangaza kufanyika kwa Kongamano la wadau kuelekea AFCON 2027 litakayofanyika Septemba 9 mwaka huu Dar es Salaam, ambapo wafanyabiashara, wawekezaji na wadau mbalimbali watapatiwa mikakati ya namna ya kushiriki kikamilifu katika fursa za kiuchumi zinazotarajiwa kuzalishwa kupitia michuano hiyo.

Mkuu huyo amewahimiza wafanyabiashara kujisajili mapema na kujiunga na mfumo wa T9 ili wasikose nafasi ya kunufaika na kile alichokiita “mapinduzi ya uchumi yatakayoletwa na AFCON 2027.

Related Articles

Back to top button