Nyumbani

Singida Black Stars kutumia Tanzanite Kwaraa

SINGIDA: BAADA ya Bodi ya Ligi Tanzania kutangaza kufungia baadhi ya viwanja kwa kutokidhi viwango, Uwanja wa CCM Liti, ambao hutumiwa na Singida Black Stars, umeathirika na kufungwa kwa muda kwa ajili ya maboresho.

Kutokana na hali hiyo, klabu hiyo imetangaza kutumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo Manyara, kwa michezo yao ya nyumbani.

Singida Black Stars wataanza rasmi kutumia uwanja huo katika mchezo wao wa Kombe la Shirikisho la CRDB (FA) dhidi ya KMC FC, utakaochezwa alhamisi, Machi 13. Uwanja wa Tanzanite Kwaraa unamilikiwa na klabu ya Fountain Gate FC, ambayo imetoa ridhaa kwa Singida Black Stars kuutumia kwa muda.

Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, amesema wamepokea taarifa ya kufungiwa kwa Uwanja wa CCM Liti na wamelazimika kufanya maamuzi ya haraka kutafuta uwanja mbadala ili kuhakikisha timu inaendelea na ratiba ya mashindano bila tatizo.

“Tunaamini ndani ya muda mfupi ukarabati wa Uwanja wa CCM Liti utakamilika na tutarudi nyumbani kucheza mechi zetu. Kwa sasa, tunalazimika kutumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kwa mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho dhidi ya KMC FC. Tumefanya maandalizi yote muhimu, na kesho timu itasafiri kwenda Manyara kwa ajili ya mchezo huo,” amesema Massanza.

Singida Black Stars ina matumaini kuwa mashabiki wao wataendelea kuiunga mkono licha ya changamoto ya uwanja, huku wakisubiri kurejea katika uwanja wao wa nyumbani mara baada ya maboresho kukamilika.

Related Articles

Back to top button