Tiger wa Tabata, Black watambiana Dar Boxing Derby

DAR ES SALAAM: BONDIA Ibrahim Paul, maarufu kama Tiger wa Tabata, amejibu tambo na vitisho vya mpinzani wake Abdullazack Hamis, anayefahamika kwa jina la Black Cobra wa Kimara, kuelekea pambano la Dar Boxing Derby litakalopigwa Julai 24, 2026, Dar es Salaam.
Akizungumza akiwa kambini Tabata Kimanga wakati akiendelea na maandalizi ya pambano hilo, Tiger amesema mchezo wa ngumi ni kama kifo kwani kila bondia hupanda ulingoni akiwa peke yake na hakuna wa kumsaidia.
Amesema siku ya pambano Black Cobra atakutana na “balaa la ulingoni”, huku akimtaka kuongeza mazoezi ili kuchelewesha kipigo anachodai kitampata.
“Namtaka afanye mazoezi ya kutosha. Siku ya pambano atakuwa peke yake ulingoni na hapo ndipo atakapojua nini maana ya kupambana na Tiger,” amesema bondia huyo kwa kujiamini.
Wakati huohuo, wadau na mashabiki wa Tiger kutoka Tabata Kimanga walionesha imani kubwa kwa bondia wao, wakidai Black Cobra ametumwa kwenye pambano ambalo litakuwa gumu kwake.
Wamesema licha ya mpinzani wao kufanya maandalizi, hawaoni akiepuka kipigo siku ya pambano, huku wakiahidi Tiger ataibuka mshindi na kuendeleza ubora wake ulingoni.




