Dulla Mbabe aomba serikali iwanusuru
BONDIA wa ngumi za kulipwa Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ ameiomba serikali iwanusuru kwa kuingilia kati mgogoro uliuopo wa wadau wa ngumi.
Miongoni mwa migogoro iliyowaathiri mabondia ni suala la Azam Media na bondia Amos Mwamakula la haki miliki wakigombea wazo la Vitasa lililosababisha kampuni hiyo kutangaza hivi karibuni kusitisha kurusha matangazo ya ngumi baada ya kushindwa kesi.
Akizungumza na gazeti hili Dulla Mbabe alisema uwepo wa mgogoro huo utawaathiri kwasababu wengi walikuwa wanategemea kuuza mapambano yao na kujipatia fedha.
“Hili suala naona serikali itusaidie kwasababu tunakoelekea tutakufa njaa, tulishazoea tunakaa kidogo tunacheza ngumi. Mdau huyu ametusaidia kuinua mchezo huu na kuonekana wenye ushindani kwa miaka ya karibuni,”alisema.
Kwa mujibu wa Dulla Mbabe, mabondia wengi wanaweza kurudi walikotoka na kujihusisha na vitendo viovu kama hatua hazitachukuliwa haraka.
Alisema serikali ina nafasi kubwa ya kuweka mambo sawa ili mdau huyo arejee kivingine kwa ajili ya kunusu mchezo wa ngumi badala ya kususia kama ambavyo amefanya sasa.
Dulla ni miongoni mwa mabondia wakongwe akiwa amecheza mapambano 50 na kati ya hayo ameshinda 35, amepoteza 14 na kupata sare moja.