Ngumi wanawake wakwama DAR

DAR ES SALAAM: Timu ya Taifa ya ngumi kwa wanawake imekwama kusafiri kuelekea Serbia kwenye mashindano ya Kombe la Dunia yaliyoanza tangu Machi 9, mwaka huu.
Hivi karibuni Baraza la Michezo la Taifa lilitangaza kuwadhamini mabondia watano kwa ajili ya kwenda kushiriki mashindano hayo makubwa.
Akizungumza na SpotiLeo Dar es Salaam leo Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) Makore Mashaga amesema kukwama huko kumesababishwa na kuchelewa kupata hati za kusafiria yaani Viza.
“Hati za kusafiria zimetoka jana, na ratiba yetu ya mashindano tulitakiwa tuanze kucheza Machi 9. Kutokana na kuchelewa tumeshindwa kuondoka,”amesema.
Amesema kutokuondoka kwa kikosi hicho wamepata hasara kubwa kwani waliweka kambi ya mwezi mzima kujiandaa na mazoezi. Pia, serikali ambayo ilitoa tiketi na wameshindwa kusafiri.
Mashaga amesema imebidi wavunje kambi waendelee na mambo mengine baada ya kukwama na safari hiyo na kujipanga zaidi kwa mashindano mengine yajayo.