Makonda: Njoeni tuenzi miaka 30 ya Bongo Fleva

DAR ES SALAAM: Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha la kuadhimisha miaka 30 ya muziki wa Bongo Fleva litakalofanyika Julai 10 Mlimani City, akisema tukio hilo si la burudani pekee, bali ni fursa ya kutafakari historia na mchango wa muziki katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza na wasanii wanaojiandaa na tamasha hilo, Makonda amesema Julai 10 inapaswa kuwa siku ya kukumbuka safari ya Bongo Fleva, kuanzia ilipoanzia hadi ilipofikia sasa.
“Tarehe 10 si mbali. Hebu tuifanye siku hiyo itukumbushe tumetoka wapi na hatua tuliyopiga. Pia, iwe nafasi ya kutathmini utunzi wa nyimbo zetu na mchango wake katika maendeleo ya taifa,” amesema.
Amesema muziki umekuwa na mchango mkubwa katika kuelimisha jamii, kuhamasisha maadili, kuheshimu wazazi, kufanya kazi kwa bidii na kuimarisha mshikamano wa Watanzania.
Makonda amesema mafanikio ya wasanii wa kizazi cha sasa, wakiwemo wanaomiliki nyumba, magari, vituo vya redio na televisheni pamoja na kuajiri watu, ni matokeo ya safari iliyoanzishwa na waanzilishi wa Bongo Fleva.
“Leo tunaona wasanii wanamiliki biashara, wameajiri vijana na wamejenga maisha kupitia muziki. Hii inaonesha kuwa sekta ya sanaa ikipewa mazingira mazuri inaweza kupunguza tatizo la ajira na kuchangia uchumi wa taifa,” amesema.
Kwa upande wake, Hamis Shaban ‘Babu Tale’ ambaye ni mdau wa muziki na Mbunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ameahidi kutoa bima za afya kwa wasanii zaidi ya 38 watakaoimba katika tamasha hilo.
Muandaaji wa tamasha hilo Hamad Ally ‘Madee’ amesema dhamira kubwa ilikuwa ni kuwarudisha marafiki zao ambao walianza pamoja nyuma kipindi cha kati wakawa wanakatishwa tamaa kwa kuitwa majina ambayo sio sahihi akitolea mfano wakongwe ambalo aliliona kama linawanyima fursa lakini sasa wamechukulia kama chalenji kuinuka tena.



