MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Aslay Isihaka amesema ukimya wake wa muda mrefu bila kutoa muziki kumetokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia ambayo hawezi
kuyasema hadharani.
Akizungumza na gazeti la HabariLEO, msanii huyo amesema pamoja na changamoto hizo lakini anapambana kuhakikisha anarudi kwenye ubora wake aliokuwa nao huko nyuma.
“Hakuna anayependa kushuka lakini sisi binadamu mara nyingi hatujui litakalotokea kesho, nimekumbana na changamoto nashukuru nimepambana zimeisha na sasa najipanga kurudi
kwenye ushindani,” amesema Aslay.
Msanii huyo amesema anaamini katika kipaji na uwezo aliokuwa nao wa kutunga mashairi yenye kuwavutia mashabiki wake hivyo itamchukua muda mfupi kabla ya kurudi kwa kasi kwenye muziki wa ushindani.
Msanii huyo amekiri kuwa ushindani wa muziki kwa sasa nchini kwetu ni mkubwa huku akimtaja rafiki yake wa karibu aliyefanya naye kazi Yamoto Bendi ya Mkubwa na Wanae chini ya Said Fella, Mbosso anayetamba akiwa na Lebo ya WCB yuko mbali kimuziki.
Msanii huyo amewaomba mashabiki wake kumpokea upya na kutarajia mambo mazuri zaidi ya ilivyokuwa huko nyuma ambako alitamba na nyimbo kadhaa ikiwemo Muhudumu, Natamba na Mchepuko.