Isarito: Wasanii tutumie Kiswahili kuitangaza Tanzania kimataifa

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu za Bongo Movie, Isarito Mwakalindile, amewataka wasanii nchini kuendelea kutumia lugha ya Kiswahili katika kazi zao za sanaa ili kuitangaza lugha hiyo pamoja na kuitangaza Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.
Akizungumza na SpotiLeo, Isarito amesema Kiswahili ni moja ya alama muhimu za utambulisho wa Tanzania, hivyo matumizi yake katika filamu, tamthilia na kazi nyingine za sanaa yana mchango mkubwa katika kuitangaza nchi na utamaduni wake duniani.
Amesema kupitia tamthilia yake ya My Son, ambayo imetumia lugha ya Kiswahili, ameweza kufikia hadhira ya kimataifa huku akichangia kukuza na kuitangaza lugha hiyo nje ya mipaka ya Tanzania.
“Tanzania ni tofauti na nchi nyingine kwa sababu ya lugha yetu ya Kiswahili. Lugha hii ni sehemu ya utamaduni na utambulisho wetu, hivyo tunapaswa kuendelea kuitumia na kuienzi kupitia kazi za sanaa,” amesema Isarito.
Ameongeza kuwa Tanzania pia imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vinavyoifanya kuwa ya kipekee, ikiwemo vyakula vya asili, tamaduni mbalimbali na ukarimu wa Watanzania ambao umeendelea kuwavutia wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa Isarito, sanaa ni moja ya njia zenye nguvu zaidi za kuitangaza Tanzania kimataifa, hivyo wasanii wanapaswa kuitumia kama jukwaa la kuonesha uzuri wa nchi, utamaduni wake na thamani ya lugha ya Kiswahili kwa dunia.
Amesisitiza kuwa kadiri wasanii wanavyoendelea kutumia Kiswahili katika kazi zao, ndivyo wanavyosaidia kueneza lugha hiyo duniani na kuongeza hamasa kwa watu wa mataifa mengine kujifunza utamaduni wa Tanzania.




