Ibenge: Uchovu ulituathiri dhidi ya Yanga

ZANZIBAR: KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema uchovu uliowakumba wachezaji wake kutokana na ratiba ya mechi kubana hatua iliyochangia kupoteza mchezo wao dhidi ya Yanga uliomalizika kwa kipigo cha mabao 3-0 jana kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar.
Akizungumza baada ya mchezo huo jana Ibenge amesema timu yake haikuanza vizuri mchezo huo na kujikuta ikiruhusu bao mapema, jambo lililowapa wakati mgumu wa kurejea kwenye mechi.
“Kama mnakumbuka, katika mchezo uliopita tulicheza tukiwa 10 dhidi ya 11. Nafikiri tulikuwa na uchovu kidogo kutokana na hali hiyo. Tuliruhusu bao moja na tukaanza vibaya,” amesema Ibenge.
Hata hivyo, amesema kadri mchezo ulivyoendelea Azam FC ilianza kurejea katika kiwango chake na hasa baada ya mapumziko ya kipindi cha kwanza.
“Taratibu tuliingia kwenye mchezo. Baada ya mapumziko tulikuwa bora zaidi, tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga na kurejea mchezoni, lakini hatukuweza kuzitumia,” amesema.
Kocha huyo alibainisha kuwa licha ya matokeo hayo, ameridhishwa na namna wachezaji wake walivyopambana hadi mwisho wa mchezo.
Ibenge amesema sasa wanaelekeza macho yao kwenye mechi zijazo huku wakijipanga kurekebisha makosa yaliyojitokeza ili kurejea katika matokeo mazuri.



