Yanga yaifanya mbaya Simba

DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga imejihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2024-2025, ikiwa ni mara ya nne mfululizo, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Simba katika mchezo wa Kariakoo Derby uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga limefungwa na Clement Mzize dakika 88 na 67 na Pacome Zouzoua, kwa mkwaju wa penalti, kufuatia kipa wa Simba, Moussa Camara, kumchezea rafu Zouzoua ndani ya eneo la hatari.
Mwamuzi wa kati kutoka Misri, Amin Mohammed Amina, hakuwa na hiyana na kuamuru mkwaju huo wa penalti.
Ushindi huo umeifanya Yanga kuondoka na pointi zote sita dhidi ya watani wao wa jadi kwa msimu huu, baada ya awali pia kushinda mchezo wa mzunguko wa kwanza kwa matokeo kama hayo. Hali hiyo imezidi kuonesha ubabe wa Yanga katika mechi za hivi karibuni dhidi ya Simba.
Kwa upande wa Simba, matokeo hayo yameongeza maumivu ya msimu kwao, kwani ni mara ya tano mfululizo wanapoteza dhidi ya Yanga, jambo linaloongeza presha kwa benchi la ufundi na wachezaji wake mbele ya mashabiki wa klabu hiyo.
Ushindi huo pia unazidi kuimarisha rekodi ya Yanga ambayo imeeendelea kuwa mwiba kwa wapinzani wake katika mechi kubwa, kikosi chake kikionekana kikiwa na nidhamu ya juu ya mchezo, ubunifu wa mashambulizi na uimara wa safu ya ulinzi.
Kwa sasa, Yanga si tu kwamba ni mabingwa wa Tanzania Bara kwa mara nyingine, bali pia wameweka wazi dhamira yao ya kutawala soka la ndani na kujenga msingi madhubuti kuelekea mashindano ya kimataifa msimu ujao.