Kwingineko

Barka Seif afungua ukurasa mpya kuelekea La Masia

BARCELONA: KIPAJI chipukizi cha soka nchini, Barka Seif, kimeandika historia baada ya kupata fursa ya kujiunga na programu ya vijana ya klabu maarufu duniani ya FC Barcelona, La Masia, hatua inayotajwa kuwa mafanikio makubwa kwa maendeleo ya soka la vijana Tanzania.

Barka, ambaye amekulia na kuendelezwa katika programu ya ukuzaji vipaji ya Magnet, amepata nafasi hiyo baada ya kuonesha uwezo mkubwa, nidhamu na kujituma katika safari yake ya soka akiwa Damm alikoibuka mfungaji bora.

La Masia inatambulika duniani kama moja ya akademi bora zaidi za soka, ikiwa imetoa nyota wakubwa waliolitumikia soka la dunia akiwemo Lionel Messi na kuendelea kuzalisha vipaji vya kizazi kipya kama Lamine Yamal.

Uongozi wa Magnet umeeleza kuwa mafanikio ya Barka ni ushahidi kuwa vijana wa Tanzania wana uwezo wa kufikia viwango vya juu zaidi vya soka la kimataifa wanapopata mazingira sahihi ya kukuza vipaji vyao.

“Safari ya Barka ni kielelezo cha kile kinachowezekana pale vipaji vinapokutana na juhudi, nidhamu na imani. Mafanikio haya si ya Barka pekee bali ni ya soka la Tanzania kwa ujumla,” ilieleza taarifa ya Magnet.

Programu hiyo ya maendeleo ya vijana imeendelea kujijengea sifa kwa kutoa fursa kwa wachezaji chipukizi kuonesha uwezo wao na kufungua milango ya mafanikio katika soka la kimataifa.

Kupata nafasi katika La Masia kunatajwa kuwa hatua kubwa kwa Barka na chanzo cha hamasa kwa vijana wengi nchini na barani Afrika wanaotamani kufikia ndoto zao kupitia mchezo wa soka.

Magnet imeeleza kuwa itaendelea kuwekeza katika ukuzaji wa vipaji vya vijana kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwasaidia kufikia viwango vya juu zaidi vya mchezo huo.

Mafanikio ya Barka Seif yanafungua ukurasa mpya katika historia ya soka la vijana Tanzania na kuonesha kuwa ndoto za kufika katika majukwaa makubwa ya dunia zinaweza kutimia kwa juhudi na maandalizi sahihi.

Related Articles

Back to top button