Kwingineko

Kisa Son, viwanja kufanyiwa uchunguzi

SEOUL:WIZARA ya Michezo ya Korea Kusini kwa kushirikiana na mamlaka ya Ligi Kuu ya nchini humo wanatarajia kufanya uchunguzi wa hali ya viwanja vyote baada ya nahodha wa timu ya taifa na nyota wa Tottenham, Son Heung-min, kulalamikia ubora wa nyasi, akidai kuwa umekuwa kikwazo kwa timu kufanya vizuri.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Michezo ya Korea Kusini, iliyochapishwa na shirika la habari la Yonhap News Agency, serikali imeahidi kuchukua hatua ikiwa ubora wa mchezo unaathiriwa moja kwa moja na hali ya viwanja.

“Tutafanya uchunguzi kisha tuje na suluhisho la matatizo yaliyoonekana, na hili tutalifanya kwa karibu sana na uongozi wa K-League pamoja na klabu shiriki. Tunatambua kuwa ubora wa viwanja ni muhimu sana iwapo tunataka kuinua kiwango cha mchezo huu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Timu ya taifa ya Korea Kusini ililazimika kuhamishia michezo yao miwili ya kufuzu Kombe la Dunia kwenye viwanja vya mikoani baada ya uwanja wao mkuu, Seoul World Cup Stadium, kuwa katika hali isiyoridhisha. Hata hivyo, malalamiko kuhusu ubovu wa viwanja nchini humo yamekuwa yakitolewa pia na wachezaji wa Ligi Kuu ya Korea (K-League).

Korea Kusini, ambao wanaongoza msimamo wa Kundi B kwenye michuano ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, wangekuwa tayari wamefuzu iwapo wangeshinda mechi zao mbili dhidi ya Jordan na Oman, lakini walitoka sare ya 1-1 katika michezo yote miwili. Hatma yao sasa itategemea matokeo ya mechi za mwezi Juni dhidi ya Iraq na Kuwait.

Related Articles

Back to top button