Tanzania yahitaji bwawa la wa watazamaji 5,000 kuimarisha mashindano ya kimataifa ya kuogelea

DAR ES SALAAM:MWENYEKITI wa Chama cha Kuogelea Tanzania, David Mwasioge, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kujengwa bwawa la kisasa lenye uwezo wa kuchukua watazamaji kati ya 3,000 hadi 5,000 ili kuwezesha Tanzania kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa na kukuza mchezo wa kuogelea nchini.
Mwasioge amesema mwitikio wa vijana kushiriki mchezo wa kuogelea unaendelea kuongezeka kila mwaka, jambo linaloonesha kuwa mchezo huo una nafasi kubwa ya kukua na kuleta mafanikio zaidi kwa taifa.
“Tumevunja rekodi ya ushiriki katika mashindano ya kuogelea. Waogeleaji wanapopata nafasi ya kushiriki mashindano makubwa hupata uzoefu zaidi na kuongeza uwezo wao wa ushindani,” amesema Mwasioge.
Amesema uwepo wa bwawa kubwa na la kisasa utasaidia kukuza vipaji vya waogeleaji wa Tanzania na kutoa nafasi kwa nchi kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa yenye ushiriki mpana na zawadi kubwa.
Mwasioge ameeleza kuwa kwa sasa watazamaji huingia bure kutokana na ufinyu wa miundombinu iliyopo, lakini hali hiyo inaweza kubadilika iwapo kutajengwa bwawa lenye uwezo mkubwa wa kupokea mashabiki wengi zaidi.
Aidha, ameitaka Serikali kushirikiana na wadau wa michezo katika kujenga mabwawa mengi ya kuogelea nchini ili kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kushiriki na kukuza vipaji vyao.
Kwa upande wake, kocha wa klabu ya Victoria, Ally Msazi, amesema waogeleaji wake wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ya kilomita tano, jambo linalothibitisha kuwa Tanzania ina vipaji vya kutosha vinavyoweza kufanya vizuri nje ya nchi.
Naye kocha wa kimataifa wa kuogelea, Alexandra, amesema mfumo mpya wa mashindano umeongeza ushindani na kusaidia kukuza kiwango cha mchezo huo kwa waogeleaji wengi.
Mashindano hayo yalishirikisha zaidi ya waogeleaji 400 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda na Mozambique, yakionesha namna mchezo wa kuogelea unavyoendelea kupata umaarufu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.




