TSA yatangaza kikosi Mashindano ya kuogelea Kanda ya tatu

DAR ES SALAAM: Shirikisho la Kuogelea Tanzania (TSA) limetangaza kikosi kitakachoiwakilisha nchi katika Mashindano ya Kuogelea Kanda ya tatu Afrika, yatakayowakutanisha waogeleaji bora kutoka mataifa mbalimbali ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuregenzi wa Elimu na Maendeleo wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) Jeremiah Keema, msafara wa Tanzania utaongozwa na Meneja wa Timu, Hadija Shebe, huku benchi la ufundi likiwa chini ya Kocha Mkuu Radhia Shaban akisaidiwa na makocha Samweli Mtupo na Rashid Kipipa.
Mashindano yatafanyika Oktoba 21 hadi 25 Oktoba mwaka huu nchini Uganda.
Kikosi hicho kinaundwa na waogeleaji wa makundi mbalimbali ya umri kuanzia miaka 12 na chini, miaka 13 hadi 14, miaka 25 hadi 16 pamoja na kundi la miaka 17 na kuendelea.
Miongoni mwa waogeleaji walioteuliwa ni Ruby Stanley, Iris Mataka, Camilla Kyenekiki, Arthur Mushi, Oscar Liebchen, Nicolene Viljoen, Ethan Makalla, Crissa Dillip, Julius Missokia, Cathleen Maokola, Abbas Abdulila na Austin Okore.
Kwa mujibu wa Shirikisho, uteuzi wa kikosi hicho mapema ni kwa ajili ya kuanza maandalizi mapema ya kujiweka imara ili sio tu kwenda kushiriki bali kupambana na kushinda.




