JKT Queens kupewa ushindi wa mezani

DAR ES SALAAM: OFISA Habari wa JKT Queens, Masau Bwire, amesema kutochezwa kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake kati ya timu yao na Ruangwa Queens kulitokana na wapinzani wao kushindwa kufika uwanjani kwa wakati uliopangwa.
Akizungumza leo baada ya mchezo huo uliokuwa ufanyike jana Mei 27 katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Bwire amesema JKT Queens ilifuata taratibu zote za mchezo kwa kufika mapema uwanjani pamoja na kukaguliwa kabla ya kuingia uwanjani tayari kwa mchezo.
“Sisi tulifika vizuri kabisa uwanjani, tukakaguliwa na kuingia uwanjani tayari kwa mchezo lakini wenzetu hawakutokea,” amesema Bwire.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa kanuni za mashindano, timu inayoshindwa kufika uwanjani baada ya taratibu zote kufuatwa hupoteza mchezo huo kwa mabao 3-0 huku timu iliyofika ikipewa pointi tatu.
“Kanuni ziko wazi kabisa, timu isipofika uwanjani na taratibu zote zikafuatwa, timu iliyofika inapewa alama tatu na mabao matatu,” amesema.
Amesema JKT Queens ilikuwa tayari kucheza kwani lengo lao kubwa ni kushindana ndani ya uwanja na kutoa burudani kwa mashabiki waliojitokeza kushuhudia mchezo huo.
“Tungependa mchezo uchezwe kwa sababu mashabiki walikuja kwa ajili ya kuona soka zuri, lakini hayo ndiyo yaliyotokea,” ameongeza.




