Ligi Ya Wanawake

Twiga Stars wamedhamiria WAFCON

DAR ES SALAAM: KIKOSI cha timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kinatarajiwa kuondoka kesho (Jumatatu) kuelekea nchini Tunisia kwa ajili ya michezo miwili ya kirafiki ya kujiandaa na fainali za kombe la mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON ) mwaka huu nchini Morocco.

Twiga Stars iliyoingia kambini Julai mosi mwaka huu inatarajia kucheza mechi hizo dhidi ya Tunisia na Botswana, kati ya Julai 8 – 16, 2024.

Akizungumza na Spotileo, Ofisa habari wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo amesema mechi hizo ni kwa maandalizi ya fainali za Mataifa ya Afrika ambayo yanayotarajiwa kufanyika nchini Morocco.

“Tunaendelea kufanya maandalizi ya timu, wanaondoka kesho (Jumatatu) kuelekea Tunisia, watacheza michezo hiyo miwili ya kujiandaa. ratiba haijapamgwa lakini tunajiandaa mapema na kujiweka tayari,” amesema Ndimbo.

Tanzania ni miongoni wa mataifa 12 ambayo bendera yake itapepea Morocco wakati timu ya soka ya wanawake ya taifa, ‘Twiga Stars’ ikishiriki kwa mara ya pili michuano hiyo.

Twiga Stars imefuzu kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya ushindi wa nyumbani wa mabao 3-0 Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kabla ya kufungwa mabao 2-0 na Togo Uwanja wa Kegue, Lome.

Kabla ya kukutana na Togo, Twiga Stars iliitupa nje Ivory Coast kwa mikwaju ya penalti 4-2, baada ya sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 180. Tanzania imeandika historia ya kufuzu kwa mara ya pili baada ya kufuzu mara ya kwanza mwaka 2010 ikiwa imepita miaka 13 tangu ilipocheza fainali za Afrika Kusini.

Tanzania ndio nchi pekee ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati iliyofuzu baada ya Kenya na Burundi kushindwa kufuzu ambapo ilitolewa na Algeria kwa jumla ya mabao 6-1 na Kenya ikifungwa na Botswana kwa jumla ya mabao 2-1.

Uganda na Kenya zimewahi kufuzu hapo awali mara moja, Uganda ikishiriki kwenye fainali mwaka 2000 na kuishia hatua ya makundi. Kenya ilipata nafasi hiyo mwaka 2016 kwenye fainali zilizofanyika Cameroon wakiwa Kundi B na kumaliza nafasi ya mwisho baada ya kushindwa kukusanya hata pointi moja.

Safari hii Watanzania watapenda kuona Twiga Stars ikicheza robo fainali au nusu na ikiwezekana fainali kwa sababu mwaka 2010 waliishia hatua ya makundi.

Related Articles

Back to top button