Zaidi ya wasanii 21,000 wasajiliwa

DODOMA: SERIKALI imeendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya sanaa nchini kwa kusajili zaidi ya wasanii 21,875 hadi kufikia Aprili 2026, hatua inayotajwa kuongeza uwazi, mipango na fursa za maendeleo kwa wadau wa sekta hiyo.
Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema ongezeko hilo ni kubwa ukilinganisha na wasanii 1,935 waliokuwa wamesajiliwa mwaka wa fedha 2024/25, likionesha mwitikio mkubwa wa wasanii kuingia kwenye mfumo rasmi.

Amesema takwimu hizo zinazokusanywa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ni muhimu katika kusaidia Serikali kupanga sera, kufanya tafiti na kuandaa mikakati ya kukuza sekta ya sanaa na ubunifu nchini.
Katika hatua ya kuendeleza vipaji na ubunifu, BASATA imefanikiwa kuratibu matukio 25 kati ya 27 yaliyopangwa kati ya Julai 2025 na Aprili 2026, sawa na utekelezaji wa asilimia 93.
Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na Bongo Flava Honors, Swahili Fashion Week, Miss Grand International, Miss Universe na matamasha ya muziki kama CIGOGO Music Festival yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Serikali imeanzisha programu ya BASATA Rising Star Award inayolenga kuibua na kukuza vipaji vya wasanii chipukizi, huku kila mwezi ikitoa tuzo kwa nyimbo bora ya msanii anayeibukia.
Pamoja na mafanikio hayo, Serikali imeweka miongozo saba ya kusimamia sekta hiyo ikiwemo ya usuluhishi wa migogoro, ulinzi wa mtoto msanii na uendeshaji wa matukio ya sanaa, hatua inayolenga kupunguza migogoro na kuongeza ubora wa kazi za sanaa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi Aprili 2026 jumla ya migogoro 20 ya wasanii imepokelewa, ambapo 10 imetatuliwa huku mingine ikiendelea kushughulikiwa kupitia dawati maalum la usuluhishi.
Katika kuhakikisha maadili yanazingatiwa, Makonda alisisitiza kuwa sanaa ni kioo cha jamii na haiwezi kuachwa bila miongozo, akibainisha kuwa maboresho ya kanuni za BASATA yanatarajiwa kuanza kutumika Julai 1, 2026.
Ameongeza kuwa pamoja na kutoa elimu kwa wasanii zaidi ya 1,400 kuhusu maadili, hatua za kinidhamu zimechukuliwa kwa baadhi ya wasanii waliokiuka taratibu.
Makonda amesema kuwa lengo la Serikali si kudhibiti sanaa bali kuiwezesha kukua kwa kuzingatia maadili, huku ikitoa fursa zaidi za kiuchumi kwa vijana kupitia ubunifu.




