EPL

Simons nje msimu mzima, kukosa pia Kombe la Dunia

LONDON, England: KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Uholanzi, Xavi Simons, ataukosa msimu uliosalia pamoja na michuano ya Kombe la Dunia 2026 kufuatia kuumia vibaya goti akiwa na klabu ya Tottenham Hotspur.

Simons, mwenye umri wa miaka 23, alipata jeraha hilo la kano ya mbele ya goti (ACL) wakati wa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wolverhampton Wanderers mwishoni mwa wiki.

Mchezaji huyo alitolewa nje kwa machela baada ya kugongana na beki wa Wolves, Hugo Bueno, kabla ya kuthibitishwa kuwa jeraha lake ni kubwa na litahitaji upasuaji.

Kupitia taarifa rasmi, Tottenham wamethibitisha kuwa Simons atafanyiwa upasuaji katika wiki zijazo kabla ya kuanza safari ndefu ya kupona, ambayo kwa kawaida huchukua kati ya miezi sita hadi tisa kwa majeraha ya aina hiyo.

Akizungumza kupitia mitandao ya kijamii, Simons amesema ameumizwa sana na hali hiyo, akieleza kuwa ndoto yake ya kuisaidia timu yake pamoja na kuiwakilisha nchi yake katika Kombe la Dunia imekatizwa ghafla.

“Nimevunjika moyo, msimu wangu umefikia mwisho ghafla na bado najaribu kuelewa kilichotokea,” alisema.

Jeraha hilo linakuja wakati mgumu kwa Tottenham ambao wanapambana kujinasua katika hatari ya kushuka daraja katika Premier League, wakiwa nafasi ya 18 na michezo michache iliyobaki.

Aidha, Simons anakuwa miongoni mwa wachezaji wengi wa Spurs waliopo majeruhi, hali inayoongeza presha kwa kikosi hicho kuelekea michezo ya mwisho ya msimu dhidi ya timu mbalimbali ikiwemo Chelsea na Everton.

Simons alijiunga na Tottenham akitokea RB Leipzig kwa ada ya pauni milioni 52 mwaka jana na amecheza mechi 28 za ligi msimu huu, akifunga mabao mawili na kutoa pasi tano za mabao.

Kwa upande wa timu ya taifa ya Uholanzi, kukosekana kwake ni pigo kubwa kuelekea michuano ya Kombe la Dunia itakayoanza Juni mwaka huu nchini Marekani, Canada na Mexico.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button