FA

JKT yawahofia Mbuni, yajipanga

DAR ES SALAAM: KOCHA wa JKT Tanzania, Ahmed Ally, amesema kikosi chake kimejipanga vizuri kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Mbuni FC, huku akisisitiza kuwa hawataidharau timu hiyo licha ya kucheza ligi ya chini.

JKT Tanzania itavaana na Mbuni FC hatua ya 16 bora kesho katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, huku Ahmed akieleza kuwa maandalizi yao yamekuwa mazuri baada ya kupata muda wa kutosha tangu walipomaliza mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo.

Amesema changamoto kubwa waliyonayo ni kucheza dhidi ya timu ambayo hawakutani nayo mara kwa mara, jambo linalowafanya wasiwe na taarifa nyingi za kiufundi kuhusu wapinzani wao.

“Maandalizi yako vizuri, tulikuwa na maandalizi ya muda mrefu kidogo baada ya kumalizika kwa mechi ya ligi dhidi ya Namungo,” amesema Ahmed.

Kocha huyo ameongeza kuwa Mbuni FC ni timu ya kupewa heshima kubwa kwa sababu mara nyingi mechi za mtoano huwa na ushindani tofauti na wa ligi.

“Tunaenda kucheza na timu ambayo kwetu inakuwa ngumu kidogo kwa sababu hatuchezi ligi moja. Wao wanacheza ligi nyingine. Ugumu unakuja wao wanatuona na sisi hatuwaoni, hatujui mapungufu yao,” amesema.

Ahmed amesema jambo muhimu kwa JKT Tanzania ni kuhakikisha wanakuwa makini katika kila dakika ya mchezo na kutumia vizuri nafasi watakazozipata.

Kwa upande wa Mbuni FC, Kocha Leonard Budeba amesema kikosi chake kiko tayari kwa pambano hilo na lengo lao ni kuonesha ushindani mkubwa pamoja na kuiheshimisha ligi ya Championship.

 

Related Articles

Back to top button