Sabilo: Simba wametufunga na mengi

DAR ES SALAAM: Mshambuliaji wa TMA Stars, Sixtus Sabilo, amesema kuwa kipigo cha mabao 3-0 walichopata kutoka kwa Simba katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB kimewapa funzo kubwa kuhusu ugumu wa Ligi Kuu Tanzania Bara na namna wanavyopaswa kujipanga kwa ajili ya kufanikisha ndoto zao za kupanda daraja.
Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa KMC Complex, ulishuhudia TMA Stars wakijitahidi kupambana lakini wakalemewa na ubora wa Simba. Hata hivyo, Sabilo anaamini kuwa uzoefu walioupata utawasaidia katika safari yao ya kuelekea Ligi Kuu.
“Kila mmoja wetu ameona tunapotaka kwenda Ligi Kuu, tunapaswa kuwa tayari kupambana, Simba wametufundisha kuwa hatuwezi kufika huko bila maandalizi mazuri na kujituma zaidi. Mechi hii imetufungua macho,” amesema Sabilo.
Mbali na kipigo hicho, Sabilo ameeleza kuwa watatumia mafunzo waliyoyapata kwa ajili ya mchezo wao ujao dhidi ya Green Warriors, ambapo watajipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
“Mchezo dhidi ya Simba ulikuwa mgumu, lakini tulijitahidi kupunguza madhara kwa kadri ya uwezo wetu, Sasa tunageuza macho yetu kwa Green Warriors, tukijua kuwa kila mechi kwetu ni hatua muhimu kuelekea malengo yetu,” ameongeza mshambuliaji huyo.