Ligi Kuu

Simba yaapa kulipa kisasi kwa Coastal Union

DAR ES SALAAM: Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema mchezo wa kesho dhidi ya Coastal Union ni miongoni mwa mechi ngumu kutokana na kumbukumbu ya msimu uliopita ambapo wapinzani hao walichangia kuinyima Simba nafasi ya kutimiza malengo yake ya ubingwa.

Ahmed amesema sare ya mabao 2-2 waliyolazimishwa na Coastal Union katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC, iliigharimu Simba kwa kupoteza alama mbili muhimu kwenye mbio za ubingwa.

Amesema kutokana na hali hiyo, Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya maumivu ya matokeo ya msimu uliopita, jambo linalowapa hamasa ya kupambana zaidi safari hii.

“Mechi dhidi ya Coastal Union kesho ni moja ya mechi ngumu kwa sababu ni miongoni mwa timu ambazo msimu uliopita zilichangia kuipoteza Simba malengo ya kuchukua ubingwa,” amesema Ahmed Ally.

Ameongeza kuwa kikosi hicho kimejipanga vizuri kwa ajili ya kurekebisha makosa yaliyojitokeza awali ili kuhakikisha hakirudii matokeo yaliyopita.

Kwa mujibu wa Ahmed, licha ya Coastal Union ya msimu huu kuwa tofauti na ile ya msimu uliopita na kuonyesha ushindani mkubwa, Simba nayo ipo katika hali nzuri na tayari kwa pambano hilo.

“Tunaingia uwanjani tukiwa na jeraha, safari hii tumejipanga vizuri kurekebisha mapungufu yetu. Tunajua Coastal ya msimu huu ni tofauti na ule uliopita, wako vizuri. Hata sisi tuko vizuri kuhakikisha tunachukua pointi tatu,” amesema.

Simba itashuka dimbani kesho kuikabili Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Jenerali Isamuhyo, ikiwa na lengo la kuondoka na ushindi ili kujiimarisha zaidi kwenye mbio za ubingwa.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button