Pamba Jiji sasa ni ya Minziro
UONGOZI wa Pamba Jiji umemtangaza kocha Fred Felix “Minziro”, kuwa kocha mkuu akichukuwa mikoba ya Goran Kopunovic aliyefutwa kazi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Ezekiel Ntibikeha ni kuwa Minziro atashirikiana na kocha msaidizi, Mathias Wandiba kukinoa kikosi cha timu hiyo katika michezo yote ya ligi kuu.
“Uongozi unawatakia kila la kheri kipindi hiki cha kazi yao mpya, tunaimani na makocha hao kufanya vizuri na kutuondoa kwenye nafasi ya chini ya msimamo, Wanamwanza wanaimani nao kuiona timu inasalia kwenye ligi,” amesema Ntibikeha.
Jumapili Oktoba 20, Minziro atakuwa uwanjani akiwa na timu hiyo itakaposhuka dimbani dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Tangu kuanza kwa msimu huu Kapunovic hajashinda mchezo hata mmoja katika saba waliyocheza, wakiambulia sare nne na kupoteza michezo mitatu huku timu hiyo ikishika mkia kwa pointi nne.