Ligi Kuu

Yanga tayari kuivaa Tanzania Prisons

DODOMA: KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, huku akisisitiza malengo yao makubwa ni kuondoka na alama tatu.

Goncalves amesema leo watafanya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo huo, huku akili za wachezaji zikiwa zimeelekezwa katika kufanya vizuri na kupata ushindi.

“Leo tutakuwa na mazoezi ya mwisho kujiandaa dhidi ya Tanzania Prisons. Akili zetu zinawaza kufanya vizuri tu na tunajua nini tunataka. Kesho tunacheza na timu ngumu ambayo imetoka kupoteza dhidi ya Simba kisha wakapata sare na Azam,” amesema Goncalves.

Amesema kutokana na mwenendo huo wa Prisons, anaamini mchezo huo hautakuwa mwepesi lakini wamefika Dodoma wakiwa na dhamira ya kupata ushindi.

Kocha huyo ameongeza kuwa licha ya kuwa na kikosi chenye wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa, ni wachezaji 11 pekee wanaoweza kuanza uwanjani lakini kila mmoja yupo tayari kuitumikia timu.

“Ninachofurahi ni kwamba wachezaji wote wana uelewa mkubwa wa mawazo yetu ya kiufundi tunayowapa. Naamini kila mmoja yupo tayari kusaidia timu. Nina imani kesho itakuwa siku ngumu lakini nzuri kwa sababu tumekuja kusaka ushindi,” amesema.

Kwa upande wake, kipa wa Yanga, Hussein Masalanga, amesema wachezaji wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo na wanatambua
umuhimu wake katika mbio za ubingwa.

“Tunajua tunaenda kucheza na timu ngumu yenye wachezaji wazuri. Tunawaheshimu, lakini kilichotuleta hapa ni pointi tatu na natumai tutazipata,” amesema Masalanga.

 

Related Articles

Back to top button