Kikapu

Makonda aitaka Dar City iandike historia mpya Afrika

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameikabidhi bendera ya taifa timu ya mpira wa kikapu ya Dar City na kuitaka kwenda kufanya vizuri katika michuano ya Afrika BAL Kalahari Conference 2026, akisema mafanikio yao yamefungua ukurasa mpya kwa mchezo huo nchini.

Akizungumza wakati akiiaga timu hiyo inayokwenda Pretoria, Afrika Kusini, kushiriki michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Machi 27 hadi Aprili 5 mwaka huu, Makonda amesema hatua iliyofikiwa na Dar City ni ya kihistoria kwa Tanzania kwani ni mara ya kwanza kwa timu ya nchini kushiriki mashindano hayo ya kiwango cha Afrika.

“Ni ukweli Dar City mmepata heshima ya kuandika historia kwa mara ya kwanza tangu mashindano haya yaanzishwe kwa Tanzania kushiriki mashindano ya Afrika. Historia mliyoandika italeta chachu na kuongeza hamasa kwa vijana wengi kuona mpira wa kikapu sio tu mchezo wa kujiburudisha, bali ni mchezo unaojenga uchumi na kubadilisha maisha ya wenye vipaji,” amesema Makonda.

Makonda aliwataka wachezaji hao kwenda kwenye michuano hiyo wakitambua kuwa Watanzania wana matumaini makubwa kwao na wanahitaji ushindi, rekodi nzuri na historia itakayobebwa na vizazi vijavyo.

Amesema mafanikio ya Dar City yanapaswa kuwa chachu kwa wadau wengine kujitokeza kuanzisha timu za kikapu ili Tanzania ipate ligi kubwa, yenye ushindani na yenye uwezo wa kufanya vizuri zaidi ndani na nje ya nchi.

Makonda alifananisha hatua ya Dar City na mchango ambao klabu za Simba na Yanga zimekuwa nao katika michuano ya kimataifa ya soka, akisema mafanikio yao yalifungua milango kwa timu nyingine za Tanzania kushiriki mashindano ya Afrika.

“Kama ambavyo Simba na Yanga walifungua milango tukaona Namungo, KMC, Azam na timu nyingine zikaingia, tunawaomba na nyinyi Dar City mkafungue milango ya kusababisha Tanzania tuwe na timu zaidi ya moja kwenda kuwakilisha Afrika,” amesema.

Rais wa Chama cha Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Hasheem Thabeet, alimshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika kuiwezesha timu hiyo kufikia hatua hiyo muhimu, huku akiomba Watanzania kuendelea kuipa sapoti Dar City katika safari hiyo ya kihistoria.

Katika michuano hiyo ya BAL Kalahari Conference 2026, Dar City itakutana na timu za Johannesburg Giants, Al Ahly ya Libya, Rwanda Patriotic Army, Nairobi City Thunder na Petro de Angola, huku ushindani mkubwa ukitarajiwa kutokana na ubora wa timu hizo katika ukanda huo.

Related Articles

Back to top button