Ibenge akubali muziki wa wachezaji wake

DODOMA: KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema ameridhishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Ibenge amesema ushindi huo ni matokeo ya juhudi kubwa na mabadiliko ya kimkakati waliyoyafanya katika michezo ya hivi karibuni, huku akisisitiza kuwa kikosi chake kinaendelea kujifunza kupambana katika mazingira tofauti ya mchezo.
“Nina furaha kwa wachezaji wangu kwa sababu walicheza mchezo mzuri sana. Tulipata sare mara mbili lakini sikuwa na wasiwasi sana. Kama ukiangalia mechi ya kwanza dhidi ya Pamba hatukucheza vizuri, lakini ya pili tulibadilisha mbinu na tukafanya vizuri zaidi. Hata tulipobaki wachezaji 10 dhidi ya 11 tuliendelea kupambana, hivyo tulijifunza namna ya kupigana hadi mwisho wa mchezo,” amesema Ibenge.
Amesema kuwa kikosi chake kinaendelea kuonesha uimara wa kisaikolojia licha ya changamoto mbalimbali, ikiwemo hali ya uwanja ambao alisema ulikuwa mgumu kuchezea katika mchezo huo.
“Tumeonesha kuwa tuna nguvu ya kiakili. Uwanja ulikuwa mgumu kuchezea lakini tulihitaji pointi tatu. Hiyo ndiyo falsafa yangu, sijali tunacheza nyumbani au ugenini, ninachotaka ni kushinda. Wachezaji wangu walikuwa bora sana hasa kipindi cha kwanza,” amesema.
Ibenge pia alieleza kuwa licha ya timu yake mara nyingi kuunda nafasi nyingi za kufunga lakini kushindwa kuzitumia vizuri, katika mchezo huo walikuwa makini zaidi mbele ya lango.
“Katika michezo mingi tulikuwa tunatengeneza nafasi nyingi lakini tunafunga chache. Leo tulitengeneza nafasi chache lakini tulizitumia vizuri moja kwa moja, tulikuwa na ufanisi mkubwa na hilo limetusaidia kudhibiti mchezo hadi mwisho,” amesema.




