JESHI Stars, TPDC zashinda Ligi ya Wavu Dar

DAR ES SALAAM: TIMU ya JESHI Stars imeibuka na ushindi wa seti 3-1 dhidi ya JKT katika mchezo wa Ligi ya Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es Salaam uliochezwa Jana.
Katika mchezo mwingine wa wanaume, TPDC iliibuka na ushindi wa seti 3-0 dhidi ya Airforce katika pambano lililoonyesha ushindani mkubwa miongoni mwa timu hizo.
Kwa upande wa wanawake, timu ya JKT ilionesha ubora wake baada ya kuifunga UDSM kwa seti 3-0 na kuendelea kujipatia matokeo mazuri kwenye michuano hiyo.
Akizungumza kuhusu michezo hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Chama cha Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es Salaam (DAREVA), Joseph Cyprian, amesema mechi zilikuwa na ushindani mkubwa hasa katika upande wa wanaume.
Amesema ushindani huo unaonesha maendeleo ya mchezo wa mpira wa wavu mkoani humo na kuwapa mashabiki burudani nzuri kila inapochezwa ligi hiyo.
Cyprian amesema michuano hiyo itaendelea tena mwishoni mwa wiki hii katika viwanja vya Chuo cha Kimataifa cha Kampala vilivyopo Dar es Salaam.




