2024 Aisha Masaka aliweka rekodi

SOKA la wanawake limekuwa sana hapa nchini, sasa tuna mwanamke wa kwanza wa kitanzania kucheza soka la kulipwa nchini England. Aisha Masaka jina ambalo limeingia kwenye rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza mwanamke kutoka Tanzania kusajiliwa na timu ya Ligi Kuu ya Wanawake ya England.
Aisha amesaini mkataba na klabu ya Brighton akitokea BK Hacken ya kutoka Sweden aliyojiunga nayo mnamo mwaka 2022 akitokea kwenye klabu ya Yanga Princess inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini Tanzania.
Mwaka mmoja uliopita Aisha aliweka rekodi ya aina yake kuwa mchezaji wa kwanza mwanamke kutoka Tanzania kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa wanawake wakati timu yake ya BK Hacken iliposhiriki michuano hiyo.
Masaka licha ya kuwa mchezaji wa kwanza mwanamke kusajili mkataba kwenye klabu hiyo anaungana na nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania Mbwana Samatta ambaye aliwahi kupita kwenye klabu ya Aston Villa mnamo mwaka 2019.
Nyota ya mshambuliaji huyo ilianza kuonekana akiwa na Alliance Girls ya mkoani Mwanza ambako alicheza kwa misimu mitatu kuanzia msimu wa 2018 hadi 2021.
Msimu uliofuata Yanga ikamsajili akitokea Alliance ambako aliwaka akawa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania msimu wa 2021/22 hivyo kushinda kiatu cha dhahabu akiweka kambani mabao 35, huku Mtanzania mwenzake, Opah Clement aliyefunga mabao 34 akiwa nafasi ya pili.
Msimu uliofuata Yanga ikamuuza kwenda Sweden ambako licha ya kutocheza kikosi cha kwanza aliweka rekodi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.