Simba Queens, Yanga Princess hapatoshi leo

DAR ES SALAAM:KOCHA Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan Mgosi amesema wachezaji wake wapo tayari kwaajili ya kutetea taji lao la Ngao ya Jamii dhidi ya mpinzani wake Yanga Princess.
Amesema Yanga Princess wamefanya usajili mzuri na wanatamani kuwa kama Simba hivyo utakuwa ni mchezo mgumu.
Mgosi amesema hayo katika mkutano wa waandishi wa habari kuelekea mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga Princess utakaochezwa Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge Dar es Salaam kesho.
“Tumefanya maandalizi mazuri, tuko vizuri lakini tutacheza kwa tahadhari kubwa kwa sababu Yanga Princess wamefanya usajili na kumrejesha Edma ambaye namkaribisha tena katika ligi ya wanawake,” amesema Mgosi.
Kwa upande wake kocha mkuu wa Yanga Princess, Edna Lema amesema kuwa ataingia kwa tahadhari kubwa katika mchezo huo.
Mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, ukiwa ni mchezo wa Dabi ya Kariakoo kwa soka la wanawake.
Lema amesema wamejiandaa vizuri anaimani watakuwa na mchezo mgumu kwa sababu ana kikosi kipya na kuandaa timu lakini anashuka dimbani kushindana.
“Simba ni timu nzuri imejipanga , hatuwaogopi bali tunawaheshimu na tunaenda kupambana kwa sababu tunahitaji kombe la Ngao ya Hisani. Mechi za dabi hizi zinatoa taswira ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania,” amesema Edna.