Nyumbani

Yanga mguu sawa 2024/25

DAR ES SALAAM: YANGA wametangaza rasmi jeshi lao litakalowapa furaha msimu ujao kwa kuwaletea Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara lakini pia kufanya maajabu Michuano ya Kimataifa.

Jeshi hilo kimetangazwa leo kwenye Tamasha la siku ya wananchi lililofanyika katika Dimba la Benjamin Mkapa, Yanga wamepata ushindi wa bao 2-1 Mchezo wa Kirafiki wa Kimataifa dhidi ya Red Arrows ya Zambia.

Bao la Red Arrows limefungwa na Rick Banda dakika ya 6.

Dakika 64 Yanga wakapata bao la kusawazisha limefungwa na Mudathir Yahya, bao la pili limefungwa na Stephane Aziz Ki dakika ya nyongeza kwa mkwaju wa penalti.

Kikosi kilichotambulishwa na Msemaji wa timu hiyo, Haji Manara kinaundwa na makipa Djigui Diarra, Abdultwalib Mshery na Aboubakar Khomeini usajili mpya akitokea Singinda Black Stars amebadilisha nafasi ya Metacha Mnata.

Wachezaji wengine ni Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Kibwana Shomari, Koussi Attohoula , Nickson Kibabage, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Chadrack Boka, Jonas Mkude, Mudathir Yahya , Faris Mussa. Khalid Aucho na Max Nzengeli.

Nyota wanaokamilisha orodha hiyo ni Salum Aboubakar, Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Shekhan Khamis, Kennedy Musonda, Denis Nkane, Clement Mzize, Clatous Chama, Prince Dube, Jean Baleke na Aziz Andambwile.

Kamanda wa Jeshi hilo ni Miguel Gamondi raia kutoka nchini Argentina ambaye ameanza vizuri msimu kwa kutwaa kombe la mashindano ya Toyota yaliyofanyika Afrika Kusini na kutarajiwa kufanya makubwa zaidi msimu wa 2024/25

Jeshi lenye uwezo wa kufanya mashambulizi ya anga na ardhini litakuwa na jukumu moja kubwa ambalo ni kuhakikisha wanatetea mataji yao na kufanya vizuri michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button