Yanga KMC mechi ya Presha

DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga leo inatarajiwa kushuka dimbani kuikabili KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa 21 utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC, huku ikiwa na dhamira ya kuendelea kulinda nafasi yake kileleni mwa msimamo wa ligi.
Yanga inaingia katika pambano hilo ikiwa vinara wa ligi kwa pointi 48 baada ya kucheza michezo 20, ikisaka kutwaa ubingwa wa tano mfululizo. Hata hivyo, pamoja na ubora wao, mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na presha waliyonayo ya kutotaka kupoteza pointi muhimu.

Kwa upande wa KMC, hali si shwari kwani wanashika mkia wa msimamo wa ligi wakiwa na pointi tisa pekee baada ya michezo 20.
Hivyo, matokeo ya mchezo huo yanaweza kuwa na athari kubwa kwa hatma yao ya kusalia au kushuka daraja, jambo linalowalazimu kupambana kwa nguvu zote.
Takwimu zinaonesha ubabe wa Yanga katika historia ya timu hizi, ambapo katika mechi 15 walizokutana, Yanga imeshinda mara 12, KMC mara moja huku sare zikiwa mbili.
Aidha, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Yanga iliibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves, amesema wanaiheshimu KMC licha ya nafasi yao kwenye msimamo, akieleza kuwa ni timu inayopambana kuepuka kushuka daraja.
Kwa upande wa KMC, Kaimu Kocha Mkuu Iman Mwalupetelo amesema kikosi chake kimejiandaa kisaikolojia kwa ajili ya pambano hilo, akisisitiza kuwa licha ya ugumu wa mchezo, wanaamini wanaweza kufanya vizuri.
Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa na ushindani mkali, kila upande ukiwa na malengo tofauti—Yanga ikisaka kuendelea kuongoza ligi na KMC ikipigania uhai wake katika Ligi Kuu.




