Wizara yaingilia kati vurugu Serie A

ROME:Wizara ya mambo ya ndani nchini Italia imepiga marufuku michezo ya Ligi kuu nchini humo Serie A kupigwa nyakati za jioni baada ya vurugu za weekend iliyopita zilizozuka katika mchezo wa Dabi ya Roma kati ya AS Roma na Lazio uliopigwa saa 3:45 usiku saa za Afrika Mashariki.
Zilizuka vurugu baina ya mashabiki wa Roma na Lazio ambao baadae waliwashambulia polisi wa kutuliza ghasia kwa vipande vya vyuma na nyundo nje ya uwanja wa Stadio Olimpico ambao ni uwanja wa nyumbani wa Lazio wenye uwezo wa kubeba mashabiki elfu 63.
“Msimu wa 2025/26 mechi zinazovuta hisia za watu wengi (High intensity matches) hazitaruhusiwa tena kuchezwa tena nyakati za jioni kama ilivyochezwa mechi ya Lazio na Roma, tunaushauri uongozi wa Serie A kutafuta muda mzuri” imesema taarifa ya Wizara
Habari zaidi kutoka nchini humo zinasema kuwa Wizara pia imewapa marufuku ya kusafiri baadhi ya mashabiki wa Lazio na Roma kwa mechi tatu zijazo za ugenini za vilabu hivyo.
Katika vurugu hizo watu 24 walijeruhiwa huku mashabiki wakubwa watatu wa Lazio na watatu wa Roma wakikamatwa.