Kwingineko

Marcelo amekubali yaishe

LONDON:BEKI wa zamani wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazili Marcelo ametangaza rasmi kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 36.

Beki huyo wa kushoto ambaye ni mmoja wa mabeki wenye hadhi zaidi Duniani alijiunga na klabu ya Real Madrid akitokea katika klabu ya Fluminense ya Brazili mwaka 2007 akiwa kijana wa miaka 18 na tangu wakati huo ameitumikia Real Madrid kwa uaminifu mkubwa.

Katika video aliyochapisha katika mitandao yake ya kijamii amesema muda alioutumia klabuni hapo ni moja ya nyakati bora sana kwenye maisha yake ya soka.

“Katika umri wa miaka 18 Madrid ilibisha hodi kwangu na nikafika hapa, sasa naweza kusema mimi ni Madrileno wa kweli. Misimu 16, mataji 25, Champions League 5, nimekuwa moja ya manahodha hapa, na nyakati nzuri zaidi ndani ya bernabeu safari yangu ya mpira inaishia hapa, japo naamini bado mpira unanidai” amesema Marcelo

Rais wa mabingwa hao watetezi wa ligi ya mabingwa barani Ulaya Florentino Peres amesema Marcelo ni mmoja ya mabeki bora zaidi kuwahi kucheza katika klabu hiyo.

Marcelo aliondoka Real Madrid mwishoni mwa msimu wa 2021-22 akajiunga na klabu ya Olympiacos ya Greece alikodumu kwa miezi 5 pekee baada ya kusaini mkataba.

Baadaye Marcelo alirejea katika klabu yake ya zamani ya nyumbani kwao Brazil Fluminense mwaka 2023 alikodumu kwa misimu miwili kabla ya kuondoka kwa makubaliano ya pande zote mbili mwezi Novemba mwaka jana.

Related Articles

Back to top button